Loading...

Mgomo walaza madereva 40 selo



MADEREVA zaidi ya 40 wa magari ya abiria aina ya Coaster zinazofanya safari kati ya Tunduma-Mbeya, wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe, wakituhumiwa kufanya mgomo.

Waliamua kugoma jana, baada ya wenzao wanne kukamatwa na trafiki na kuwaweka rumande kwa madai ya kupakia abiria eneo la Mwaka katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba, ambalo sio rasmi.

Baada ya kukamatwa kwa madereva hao, chama cha madereva mkoani Songwe kiliitisha mgomo wa kulishinikiza jeshi hilo kuwaachia huru wenzao.

Atupele Mwamunyange, dereva alisema chanzo cha kugoma ni kutokana na Jeshi la Polisi kutumia mguvu kubwa kuwakamata wenzao bila kuwatoza faini baada ya kuwatuhumu kuegesha magari na kupakia eneo ambalo haliruhusiwi.

Dereva mwingine, Fredi Kamali, alisema wanashindwa kutimiza malengo ya mapato ya matajiri wao kutokana na kuwapo kwa tozo za faini zisizo rafiki na kuwa wanapodai risiti wanajenga uadui na askari.

Godfrey Ibrahim, kondakta, alisema wakiwa safarini kutoka Mbeya wakikaribia kufika Tunduma wanapata hofu kubwa kutokana na trafiki kuwatoza faini za kuwatafutia makosa na kuiomba serikali kuliona tatizo hilo.

Andrew Mwakikunda, Mwenyekiti wa chama cha madereva mkoani humo, alisema hawako tayari kuingiza magari yao barabarani hadi wenzao waliokamatwa watakapoachiwa huru na kuwa wanahitaji kufanya mazungumzo na mkuu wa mkoa.

“Haiwezekani tuonekane wauzaji wa bangi kwa kukamatwa ovyo wakati tunafanya kazi halali ya kuliingizia Taifa kipato na familia zetu zikiishi kwa kazi hii,” alisema Mwakikunda. 

Anna William, abiria, alisema kukosekana kwa magari kumewasababishia adha ya kukosa usafiri hasa kwa wanaokwenda hospitalini kutibiwa na wengine kupata mahitaji muhimu.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoani Songwe, Faidhi Tukamazila, alisema madereva waliokamatwa wamekiuka taratibu za mkataba na kuwa walisaini makubaliano ya kusafirisha abiria, lakini wamefanya mgomo kinyume cha makubaliano.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mathias Nyange, licha ya kukiri kuwapo kwa mgomo huo, alisema ni kinyume cha makubaliano kwa kuwa askari wake walikamata magari manne kwa kosa la kuegesha magari eneo lisilo rasmi.

Alisema kutokana na madereva hao wanne kutozwa faini mara kwa mara, Jeshi hilo liliamua kuwapeleka mahakamani ili wapate funzo la kutofanya makosa.
Aidha, Kamanda Nyange alisema kutokana na mgomo huo, wamewakamata madereva wengine 40 na watafikishwa mahakamani leo.
Mgomo walaza madereva 40 selo Mgomo walaza madereva 40 selo Reviewed by Zero Degree on 6/20/2017 11:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.