Loading...

Rita yaeleza sababu za kuitambua bodi ya wadhamini ya Prof. Lipumba


Profesa Ibrahim Lipumba ameunda kamati ya maadili na nidhamu kwa ajili ya kuwahoji wanachama watovu wa nidhamu, katika siku ambayo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umeeleza sababu za kuitambua bodi ya wadhamini ya msomi huyo.

Profesa Lipumba anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa mwenyekiti wa CUF, lakini anapingwa vikali na upande unaoongozwa na katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ambao unasema alishajiuzulu uenyekiti na Mkutano Mkuu kuridhia.

Jana ofisa mtendaji mkuu wa Rita, Emmy Hudson aliiambia Mwananchi kuwa aliisajili bodi hiyo mpya baada ya kupata uthibitisho wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa upande wa Profesa Lipumba ndio unaotambulika na ofisi yake.

Hudson alisema kwa kifupi kuwa walipokea maombi ya kusajili bodi ya wadhamini Machi 23 kutoka pande zote mbili, lakini hawakuyafanyia kazi siku hiyo.

Alisema walianza kushughulikia maombi hayo taratibu na baadaye kuomba uthibitisho kwa Msajili kuhusu upande ambao unatambulika.

“Baada ya kuzungumza na pande zote mbili, baadaye msajili alisema anautambua upande wa Lipumba. Tulifuatilia taarifa kwa msajili kwa kuwa ndiye mwenye dhamana. Sisi sote turudi kwa msajili atuambie kwa nini anamtambua Lipumba na siyo Maalim,” alisema Hudson. 

Juni 22, CUF upande wa Profesa Lipumba uliitambulisha rasmi bodi mpya ya wadhamini wakidai kuwa imesajiliwa na Rita Juni 12. Pia, walieleza kuwa kusajiliwa kwa bodi hiyo kunaifanya CUF iwe moja na kuondoa migogoro yote iliyoigawa.

Mgogoro ndani ya CUF ulianza baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti na nyadhifa nyingine zote Agosti 2015 na mwaka mmoja baadaye kurudi akitaka kuendelea na nafasi yake.

Lakini mkutano mkuu wa CUF ulioitishwa mwaka jana ulikataa maombi yake ya kurudi katika nafasi ya uenyekiti na kumtaka afuate taratibu kwa kugombee uongozi huo. Mkutano huo ulikubaliana na uamuzi wa kujiuzulu na kuunda kamati ya uongozi iliyo chini ya Julius Mtatiro, jambo ambalo Profesa Lipumba hajakubaliana nalo.

Hata hivyo, baada ya pande hizo mbili kukaa na Msajili, ofisi hiyo iliandika barua ya kueleza kuwa inamtambua mchumi huyo kuwa mwenyekiti halali.

Jana, Profesa Lipumba aliongea na waandishi wa habari kuwaeleza hatua ambazo chama chake kinachukua dhidi ya wanachama aliowaita kuwa ni watovu wa nidhamu.

Profesa Lipumba aliorodhesha makosa manne ambayo Maalim Seif anatakiwa kuyajibu atakapohojiwa na kamati hiyo kuwa ni kutoonekana ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni kwa kipindi kirefu na kwa kufanya hivyo amekwenda kinyume na katiba inayomtaka kuhudhuria ofisini na kuitisha vikao vya chama kadri inavyowezekana.

“Kamati mtaanza na hili, maana huyu mtendaji mkuu wa chama hajaonekana hapa ofisini kwa kipindi kirefu na amekuwa akipuuza maelekezo yangu yote. Hivyo lazima aitwe ahojiwe, ajieleze na kisha mapendekezo yenu tuleteeni Baraza Kuu,” alisema. 

Kosa jingine alilolitaja ni kushirikiana na viongozi wa Chadema kuidhoofisha CUF upande wa Tanzania Bara.

Alisema Maalim Seif yuko karibu na viongozi wa Chadema na hata wakati mwingine kuwapa nafasi kuwa wasemaji wa mambo yanayohusu CUF.

Profesa Lipumba alisema kitendo hicho kinadhalilisha chama chao na kufanya kipoteze mwelekeo mbele ya wanachama.

Pia, ameorodheshewa kosa la kwenda kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Baraza Kuu lililomtaka kufungua mashtaka mahakamani kupinga kufutiwa matokeo kwa wawakilishi katika uchaguzi uliopita.

Alisema chama kiliazimia kupinga kitendo cha kufutwa kwa matokeo ya wawakilishi wake 27 ambao walitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa washindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi mgombea akishatangazwa ameshindwa huwezi kufuta tena matokeo na kwa maana hiyo tulimuagiza aende mahakamani akatetee hoja hii, lakini yeye hakufanya na kwa jinsi hiyo tumepoteza majimbo yote 27. Lazima sasa ajieleze,” alisema Profesa Lipumba. 

Pia, Maalim Seif anakabiliwa na kosa la kutoa matamshi yanayokinzana na misingi na falsafa za chama kama vile suala linalohusu Muungano ambalo Profesa Lipumba alisema msimamo wa chama hicho kuhusu Muungano unaeleweka wazi ukiwa umejikita katika Ripoti ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1992 unaosisitiza kuwepo kwa mfumo wa shirikisho wa Serikali tatu.

Katika kosa hilo, Lipumba alisema Maalim Seif amekiuka msingi huo kwa kutoa matamshi yanayotaka kuwepo kwa Serikali ya mkataba.

“Katibu mkuu ndiye mtendaji wa chama, lakini mwenzetu wakati alipokwenda Tume ya Jaji Warioba alisema anataka Serikali ya mkataba. Matamshi haya si tu yanaathiri chama, bali yanaathiri nchi,” alisema. 

Alisema kiongozi huyo amekuwa hampi ushirikiano wowote naibu katibu mkuu upande wa Tanzania Bara, Magdalena Sakaya na kwa kufanya hivyo amevunja katiba ya chama hicho.

Mwingine anayetakiwa kuhojiwa ni naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ambaye anatuhumiwa kutoa matamshi ya kumdhihaki mwenyekiti wa chama na kupokonya madaraka ya Sakaya.
Rita yaeleza sababu za kuitambua bodi ya wadhamini ya Prof. Lipumba Rita yaeleza sababu za kuitambua bodi ya wadhamini ya Prof. Lipumba Reviewed by Zero Degree on 6/25/2017 10:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.