Loading...

Uhalifu unavyozidi kushika kasi Kibiti


VITENDO vya uhalifu katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani vimeendelea kushika kasi baada ya watu watatu kutekwa juzi usiku kwa mbinu za ‘kimafia’ huku Jeshi la Polisi likitangaza kuanza msako mkali wa kujua walipo watu hao na pia kuwatia mbaroni watekaji.

Tukio hilo la utekaji ambalo ni la pili mfululizo katika kipindi cha chini ya wiki moja, lilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Nyamisati wilayani Kibiti, ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa matukio ya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia na pia utekaji, ambayo hadi sasa wanaoyatekeleza hawajajulikana ni watu gani na lengo lao ni lipi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Onesmo Lyanga, alisema kuwa tukio hilo la kutekwa kwa watu watatu lilitokea usiku wa kuamkia jana na pia jingine lilitokea siku moja kabla, hivyo kuwapo kwa jumla ya watu wanne waliotoweka na hadi sasa hawajulikani walipo.

Akisimulia namna tukio la usiku wa kuamkia jana, Kamanda Lyanga alisema lilitokea katika mazingira yanayoacha maswali mengi baada ya watekaji kuvamia nyumba za wahusika, eneo la Nyamisati, Wilaya ya Kibiti.

Kamanda Lyanga alisema waliotekwa katika tukio la usiku wa kuamkia jana ni wanaume wawili na mwanamke mmoja.

“Mmoja kati ya wanaume hawa ni mpenzi wa mwanamke ambaye naye hajulikani alipo. Kwa mujibu wa watu wanaowafahamu, tukio hilo lilitokea (wakati) wakiwa nyumbani kwao,” alisema. 

Kamanda Lyanga alisema kutoweka kwa watu hao kunafikisha idadi ya watu waliotekwa kuwa wanne baada ya tukio lingine lililotokea Jumatano, likimhusisha Mwenyekiti wa Kijiji cha Kati, Wilaya ya Ikwiriri, Athumani Mtoteka. Yeye (Mtoteka) alivamiwa nyumbani kwake usiku na kuchukuliwa kinguvu na watu wasiojulikana ambao walimpeleka kusikojulikana.


“Tunaendelea kuwasaka kupitia vikosi vyetu vya polisi…hadi sasa bado hatujafahamu sababu za wahalifu hawa kufanya vitendo hivi,” alisema Kamanda Lyanga.

VIFO ZAIDI YA 30

Mfululizo wa matukio ya mauaji, kujeruhi na kuteka yalianza tangu Mei mwaka jana na hadi sasa, watu zaidi 30 wameripotiwa kupoteza maisha, miongoni mwao wakiwamo viongozi wa vijiji na vitongoji, askari mgambo, makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia askari wa jeshi la Polisi.

Miongoni mwa matukio ya mauaji na mashambulizi yaliyotokea hivi karibuni ni la kujeruhiwa kichwani kwa mkulima aliyepigwa risasi na pia lingine lililotokea Jumatatu wakati watu wasiofahamika walipomuua mwananchi mmoja, mkazi wa Ikwiriri.

Katika njia mojawapo ya kutafuta dawa ya kumaliza uhalifu huo, mkuu mpya wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, alitembelea Kibiti wiki iliyopita na kuzungumza na wazee kadhaa kuhusiana na hali ya usalama na amani katika wilaya hiyo na nyingine za mkoa wa Pwani.
Uhalifu unavyozidi kushika kasi Kibiti Uhalifu unavyozidi kushika kasi Kibiti Reviewed by Zero Degree on 6/10/2017 09:57:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.