Loading...

Mwalimu wa Sekondari matatani kwa kumpa mimba mwanafunzi wake


Mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Miangalua wilayani Sumbawanga, Rukwa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wake wa kidato cha tatu.

Mkuu wa shule hiyo, Gishi Milundi amekiri kuwa ni kweli mwanafunzi wake ambaye anasoma kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 16 ni mjamzito na anadai kuwa amepewa ujauzito huo na mwalimu wake na tayari mwalimu huyo amekamatwa na polisi wa Kituo cha Laela.

Amesema kuwa baada ya kuhisi kuwa mwanafunzi huyo ni mjamzito alipelekwa katika zahanati ya Kijiji cha Miangalua na alipopimwa akabainika ana ujauzito wa miezi mitano na yeye binafsi alishamuonya mwalimu huyo na tabia ya kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi. 

“Nilikuwa namuonya lakini hakusikia mpaka alipompa ujauzito na kumsababishia kukatisha masomo kutokana na hali hiyo,’’ amesema.

Mkuu huyo wa shule alisema yeye hana la kufanya isipokuwa ameliachia Jeshi la Polisi ili lichukue hatua kwa kuwa kitendo alichofanya mwalimu huyo ni kosa kisheria na tayari ameshamtoa shuleni hapo mwanafunzi huyo kwa kuwa sheria haimruhusu kuendelea na masomo akiwa mjamzito.

Mzazi wa mwanafunzi huyo, (jina tunalo) aliyezungumza na gazeti hili alikiri kuwa mtoto wake ni mjamzito na kwa sasa ameacha kwenda shule na kila anapoulizwa anadai ujauzito huo aliupata kwa mwalimu ambaye wamekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu.

Amesema kuwa kinachomsikitisha ni kuona kuwa mtoto wake huyo amepoteza fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari kwani Serikali ilishapiga marufuku wanafunzi waliojifungua kurejea shuleni.

Mzazi huyo pia alidai hana mpango wa kumsomesha tena kwa kuwa uwezo wake ni mdogo kwani amechezea fursa ya kusoma shule za Serikali itabidi akae tu nyumbani kwani hana kipato cha kumsomesha hata chuo cha ufundi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando, amesema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.

Alisema kwamba mtuhumiwa anatuhumiwa kwa makosa ya kumpa mimba mwanafunzi na kumbaka kwa kuwa mwanafunzi huyo ana umri wa chini ya miaka 18.
Mwalimu wa Sekondari matatani kwa kumpa mimba mwanafunzi wake Mwalimu wa Sekondari matatani kwa kumpa mimba mwanafunzi wake Reviewed by Zero Degree on 7/21/2017 06:45:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.