Loading...

Polisi waua watuhumiwa wawili katika msitu wa Ngomboroni Kibiti


Jeshi la Polisi nchini limewaua watu wawili wanaodaiwa kufanya mauaji katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, mkoani Pwani.

Akielezea tukio hilo leo (Alhamisi Julai 6) , Mkuu wa Operesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas amesema tukio hilo lilitokea jana saa nne usiku katika msitu wa Ngomboroni Kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri.

Wahalifu hao waliuawa na askari wa operesheni maalumu wakiwa katika doria za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea katika kanda hiyo ya kipolisi.

Alisema askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika mauaji hayo ambaye alikamatwa, alikubali kwenda kuwaonyesha polisi mahali ambapo ni maficho ya wenzake.


“Baada ya kufika eneo la msitu wa Ngomboroni kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi naye alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili,” amesema. 

Ameongeza; “majeruhi hao wawili walifariki dunia njiani wakati wakipelekwa hospitali kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.” 

Kamishna Sabas amesema katika tukio hilo wamefanikiwa kupokonya silaha mbili aina ya SMG na Shotgun moja pamoja na risasi tisa.

Kamishina Sabas amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia na kwamba zawadi nono bado ipo pale pale na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wahalifu wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya Rufiji.
Polisi waua watuhumiwa wawili katika msitu wa Ngomboroni Kibiti Polisi waua watuhumiwa wawili katika msitu wa Ngomboroni Kibiti Reviewed by Zero Degree on 7/06/2017 07:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.