Loading...

Taifa Stars kuanza safari ya kusaka tiketi ya CHAN dhidi ya Rwanda (Amavubi) leo hii


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga, amesema kuwa kikosi chake kitaivaa Rwanda (Amavubi) kwa nguvu bila kujali rekodi ya matokeo waliyopata katika mechi zilizopita hivi karibuni kwenye michuano ya Kombe la Cosafa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza mazoezi ya asubuhi kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba, Mayanga alisema kuwa amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha leo wanaanza vyema safari ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Mayanga alisema kuwa kikubwa katika mazoezi yake alikuwa anawajenga wachezaji kiakili na kujipanga kutowadharau wapinzani wao ambao nayo wanataka kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo ya kwanza ya ugenini.

"Tunashukuru tumemaliza mazoezi ya mwisho asubuhi hii (jana asubuhi) kazi kubwa benchi la ufundi lilikuwa pia kuondoa uchovu walioupata katika mechi zilizopita na pia tumewaandaa wachezaji kuikabili Rwanda bila ya kuwa na kumbukumbu ya historia ya mechi zilizopita, tunajua Rwanda ina wachezaji wenye kasi na wenye morali ya kijeshi," alisema Mayanga. 

Kocha huyo aliongeza kuwa hana majeruhi katika timu yake na tayari wote wamepata nafasi ya kuangalia video ya mechi yao ya mwisho kwa lengo la kuwapeleleza.

"Rwanda haina mabadiliko sana, tutaingia uwanjani kwa kazi moja tu ya kuhakikisha tunashinda na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hii," aliongeza Mayanga, kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Morogoro na Tanzania Prisons ya Mbeya. 

Nahodha wa Taifa Stars, Himid Mao, alisema kuwa kila mchezaji amejiandaa kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi katika mechi ya leo.

"Ni mechi muhimu na ngumu kwa kila upande, ila tutahakikisha tunajituma na kushinda katika mchezo huu hapa nyumbani, tunaomba Watanzania waendelee kutuombea ili malengo yetu yatimie," alisema kiungo huyo. 

Kikosi cha Amavubi kimeshatua jijini hapa na jioni kilifanya mazoezi tayari kuwakabili wenyeji.

Timu hizo zinatarajia kurudiana Julai 23 mwaka huu jijini Kigali Rwanda na mshindi wa jumla atakutana na Uganda (Cranes) au Sudani Kusini.
Taifa Stars kuanza safari ya kusaka tiketi ya CHAN dhidi ya Rwanda (Amavubi) leo hii Taifa Stars kuanza safari ya kusaka tiketi ya CHAN dhidi ya Rwanda (Amavubi) leo hii Reviewed by Zero Degree on 7/15/2017 09:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.