Loading...

India: Madaktari wagombana wakati walipokuwa wakimfanyia mgonjwa upasuaji


Picha ya madaktari wawili wakikorofishana wakati walipokuwa wakimfanyia mgonjwa upasuaji, imesambaa katika mitandao ya kijamii.

Madaktari hao wawili wamesimamishwa kazi kwa muda nchini India, baada ya video kusambaa mitandaoni wakigombana vikali, huku wakiwa wamesimama kandokando ya mama mmoja mja mzito, wakati wa upasuaji.

Taarifa kutoka Hospitali hiyo imethibitisha kuwa wawili hao wamesimamishwa kazi kwa muda.

Video ya kisa hicho kilichotokea katika Hospitali ya Umaid iliyoko kaskazini mwa mji wa Rajasthan, imesambazwa pakubwa na kusababisha malalamishi makubwa.

Afisa mmoja mkuu wa Hospitali hiyo ameiambia BBC kuwa, mwanamke aliyekuwa akifanyiwa upasuaji na mwanawe wako salama.

Chanzo cha video hiyo bado haijabainika, lakini wakuu wamethibitisha kuwa kisa hicho kilifanyika hospitalini humo.

Matusi mtandaoni
Mara baada ya kuonekana kwa mkanda huo wa video mtandaoni, ripoti nyingi ilidai kuwa mwanamke anayeonekana akiwa katika meza ya upasuaji alimzaa mtoto ambaye alifariki baadaye.

Lakini Dkt Ranjana Desai, mkuu wa Hospitali hya Umaid mjini Jodhpur, amekanusha madai hayo na kusema mtoto na mamake wako salama.

''Wakati nilipoina video hiyo, na kufanya uchunguzi wa ndani kwa ndani, vyombo vya habari tayari vilikuwa vimetangaza kuwa, mtoto huyu alikuwa amefariki," aliiambia BBC.

Kuna mtoto amefariki lakini siye ambaye vyomo vya habari vilitangaza, amesema.

Mita chache kutoka hapo, kwenye meza nyingine ya upasuaji, kwenye chumba hicho hicho hospitalini, mama mwingine alizalishwa mtoto ambaye alikuwa amefariki tayari.

"Visa hivi viwili havina uhusiano hata kidogo," Dkt Desai aliiambia BBC.

Kwenye Video, ambayo imesambazwa pakubwa mitandaoni, madaktari wawili wanasikika wakirushiana matusi mazito mazito kwa lugha ya Kihindi, na kuanza baadaye kugombana ikiwa mgonjwa huyo alikuwa amekula kabla ya upasuaji.

Dkt Desai amewatambua madaktari hao wawili na kutaja majina yao kama Dkt Ashok Nanival na Dkt Mathura Lal Tak.

Amesema kuwa madaktari hao hawajafutwa kazi bali wamesimamishwa tu kazi kwenye Hospitali hiyo, huku mamlaka kuu ya Hospitali hiyo ikiendeleza uchunguzi dhidi ya kisa hicho.

Mahakama kuu ya jimbo la Rajasthan imeamuru Hospitali hiyo kutoa ripoti ya kina, huku mahakama hiyo ikitekeleza uchunguzi wao kuhusiana na kisa hicho.
India: Madaktari wagombana wakati walipokuwa wakimfanyia mgonjwa upasuaji India: Madaktari wagombana wakati walipokuwa wakimfanyia mgonjwa upasuaji Reviewed by Zero Degree on 8/30/2017 11:11:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.