Loading...

Mufti: Mafundisho yaliyo nje ya maadili ya dini ya Kiislamu hayana nafasi ndani ya Bakwata

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir
MUFTI wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir Bin Ally amesema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) halitawavumilia wale wote wanaotumia dini Kiislamu kueneza mafundisho yaliyo kinyume na maadili ya Uislamu.

Shehe Zubeir alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa madrasa na maktaba ya chuo cha Izzadini, vilivyoko eneo la Njoro, Manispaa ya Moshi, ambapo pia alichukua fursa hiyo kuwatakia Wakristu heri ya Sikukuu ya Krismasi.

“Mafundisho yaliyo nje ya maadili ya dini ya Kiislamu hayana nafasi ndani ya Bakwata na yaungwe mkono na mtu yeyote kwa nia yoyote na tutaendelea kuyakemea haya”, alisema.

Alisema siku zote Bakwata inasisitiza mafundisho ya kidini yafanyike ili mradi watu wapate elimu kuanzia ngazi za chini na kwamba wale watakaobainika kutumia nafasi hizo vibaya watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha alisema Bakwata itaendelea kupiga vita fikra potofu ambazo zimekuwa zikienezwa na mafundisho yanayolenga kuwaharibu Waislamu hasa vijana ambao ndiyo nguzo ya Uislamu katika miaka ya baadaye.

“Mimi ninakemea kwa nguvu zote mafundisho ya aina hii kutolewa hapa nchini na wale wanaotoa mafundisho ya namna hii wakijulikana wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Shehe Khamis Mataka, alipongeza ujenzi wa maktaba na madrasa ambazo alisema ni msingi bora katika kukuza maadili ya watoto wa kiislamu.
Mufti: Mafundisho yaliyo nje ya maadili ya dini ya Kiislamu hayana nafasi ndani ya Bakwata Mufti: Mafundisho yaliyo nje ya maadili ya dini ya Kiislamu hayana nafasi ndani ya Bakwata Reviewed by Zero Degree on 12/25/2017 07:17:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.