Loading...

Thierry Henry akanusha kumshauri Sanchez aihame Arsenal


Mchezaji maarufu wa zamani wa Arsenal Thierry Henry amekanusha kwamba alimwambia Alexis Sanchez aihame klabu hiyo na kujiunga na Manchester United.

Sanchez, aliyejiunga na United Jumatatu kwa makubaliano ya kubadilishana wachezaji ambapo Henrikh Mkhitaryan alihamia Arsenal, amesema alikuwa amezungumza na Mfaransa huyo.

"Nakumbuka leo, mazungumzo niliyokuwa nayo na Henry, ambaye alibadilisha klabu kwa sababu sawa na leo ni zamu yangu," Sanchez aliandika kwenye Instagram.

Henry, aliyehamia Barcelona mwaka 2007, alijibu Jumanne na kusema: "Hakuna wakati hata mmoja ambao nilimwambia Alexis Sanchez aondoke Arsenal."

Akijibu shutuma dhidi yake, Henry, ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji mabao Arsenal aliongeza kwenye ujumbe wa Twitter kwamba: "Sikuwa na habari kwamba alikuwa ahajiunga na Man Utd hadi nilipoona kwenye vyombo vya habari sawa nanyi."

Henry, 40, alihamia Nou Camp baada ya kukaa misimu minane katika klabu ya Arsenal kwa uhamisho uliogharimu pauni milioni 16.1.

Akiwa Barca alishinda mataji mawili ya La Liga na kombe moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Sanchez, 29, kutoka Chile alikaribia kuhamia Manchester City mwezi Agosti mwaka jana lakini ikashindikana, na sasa ametia saini mkataba wa miaka minne  na nusu katika klabu ya Manchester United ambapo atakuwa analipwa pauni milioni 14 kwa mwaka baada ya kutozwa ushuru.
Thierry Henry akanusha kumshauri Sanchez aihame Arsenal Thierry Henry akanusha kumshauri Sanchez aihame Arsenal Reviewed by Zero Degree on 1/25/2018 12:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.