Loading...

Udom kutoa elimu ya watu wazima

CHUO CHA UDOM
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimezindua mpango maalum wa kutoa mafunzo ya elimu ya watu wazima katika vijiji vinavyozunguka chuo kicho.

Mpango huo ulizinduliwa na aliyekuwa Makamu Mkuu wa Udom, Prof. Idris Kikula katika Shule ya sekondari Ng’ong’ona, jirani na chuo hicho.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Prof. Kikula alisema wazo la kuanzisha mpango huo lilikuwapo tangu siku nyingi, lakini mwaka huu wameamua kuzindua rasmi ili kuwasaidia wananchi waliokosa elimu wanaoishi jirani na eneo hilo.

“Imefika kipindi ambacho vyuo vikuu vinatakiwa kufanya mageuzi kwa kushuka chini na kuwasaidia wananchi katika elimu ya chini ili kukamilisha dhana ya kuelimisha,” alisema Prof. Kikula. 

Hata hivyo, alisema waliamua kutekeleza mpango huo kutokana na utafiti uliofanywa na chuo hicho kubaini kuwa kuna baadhi ya wananchi wa vijiji jirani na chuo hawajui kusoma na kuandika.

Alisema waliona kuwa wanajukumu la kuwasaidia wananchi hao ili waweze kunufaika na uwepo wa chuo hicho jirani.

Alisema kuwa kampeni hiyo ya kutoa elimu kwa watu wazima wameipa jina la ‘Tokemeza saini ya kidole gumba’ ikiwa na lengo la kila mwananchi asiyejua kusoma na kuandika apate elimu hiyo inayotolewa bure na chuo hicho.

Mkuu wa mpango wa mafunzo hayo, Dk. Joseph Manase akitoa taarifa, alisema mpango huo umeanza Machi 5, mwaka huu na hadi Machi 14, wameshaandikisha wanafunzi watu wazima 81, wanawake 52 na wanaume 29.

Aidha, alisema pamoja na kuendesha darasa la watu wazima, pia wamefungua darasa la watoto waliokosa elimu ya msingi ili nao wafaidike na mpango huo.

Alisema wanatumia vyumba vya madarasa ya Shule ya Sekondari ya Ng’ong’ona na muda wa masomo unaanza majira tisa hadi saa 12 jioni.

Aidha, alisema katika mpango huo, wanawatumia wanafunzi wa chuo hicho wa elimu pamoja na baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho kwa kujitolea.

Mmoja wa wanafunzi wa darasa hilo, Emmanuel Lucas (41), aliwashukuru Udom kwa kuanzisha mpango huo wa kuwasaidia wananchi wanaoishi jirani na chuo hicho.

“Mimi binafsi mnavyoniona hapa nilikuwa sijui kuandika hata A, lakini baada ya kuingia darasani kwa siku chache hizi sasa ninaweza kuandika jina langu pamoja na kusoma maandishi mimi mwenyewe bila kusomewa na mtu,” alisema Lucas. 

Aliomba chuo hicho kuwa na mpango endelevu wa kuwasaidia wananchi hao kupata elimu ambayo waliikosa.
Udom kutoa elimu ya watu wazima Udom kutoa elimu ya watu wazima Reviewed by Zero Degree on 3/18/2018 03:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.