Loading...

Ajali ya Noah yaua watu nane mkoani Mbeya


Watu nane wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugongana uso kwa uso na basi la abiria mapema hii leo mkoani Mbeya.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Musa Athumani Taibu, amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 5 asubuhi ambapo imehusisha gari aina ya Noah lene namba za usajili T649 EEA ilipogongana uso kwa uso na basi la abiria la Ijembesabo lenye namba za usajili T 672 CLR, linalofanya safari zake Mbeya mjini na Chunya.

Kamanda Taibu amesema chanzo cha ajali hiyo ni basi hilo kuacha njia yake na kuingia upande mwengine, ndipo lilipogongana uso kwa uso na noah hiyo ambayo ilikuwa imebeba watu waliokuwa wakienda msibani Mbeya Mjini.

"Ajali imetokea leo asubuhi saa 5 barabara ya Mbeya - Chunya eneo la maili tano, Noah ilikuwa ya watu binafsi na ilikuwa imebeba abiria 9, ilikuwa inatoka Chunya kuja Mbeya Mjini Msibani, chanzo cha ajali ni huyu dereva wa basi kubwa aliondoka kwenye site yake na kugongana na Noah, kwenye noah wamekufa nane, wanaume watatu, wanawake watano, aliyenusurika ambaye ni majeruhi ni mwanamke mmoja, dereva wa Noah ametambulika kwa jinala Juma Lihinda wa Chunya amefariki papo hapo, waliotambulika ni Husna Lusambo, Jackline Charles, na Alphateri Niyaba maarufu kama Mkosa sura, wote wakazi wa Chunya”, amesema Kamanda Taibu.

Kamanda Taibu amesema miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali mkoani Mbeya, na dereva wa basi la abiria aliyetambulika kwa jina moja la Abdallah anatafutwa na polisi kwani alikimbia baada ya ajali, ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ajali ya Noah yaua watu nane mkoani Mbeya Ajali ya Noah yaua watu nane mkoani Mbeya Reviewed by Zero Degree on 4/09/2018 11:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.