Loading...

Spika ataka DNA za waliozaa na Wabunge


Spika wa Bunge la Tanzania , Job Ndugai amewataka kina mama wenye malalamiko ya kutelekezewa watoto na wabunge wafike kwake au wamwandikie barua kuhusu suala hilo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha cheti cha uthibitisho cha vipimo vya vinasaba (DNA) ili kushughulikia suala hilo.

Hayo yamesemwa na Mh. Ndugai wakati akiahirisha kikao cha sita cha Bunge mjini Dodoma ambapo alitoa taarifa kwa Wabunge na kuwaambia kuwa zoezi linaloendelea Dar es salaam limetikisa kiti chake na kwamba wapo Wabunge ambapo wanetuhumiwa.

“Kule Dar es Salaam kuna zoezi linaendelea, huko sasa kidogo kiti cha Spika kimetikiswa hivi. Tunatuhumiwa mahali, kidogo tumeguswa hivi kwa hiyo natarajia kupata ushauri wenu waheshimiwa tunafanyaje katika mazingira haya kwa maana kuna watoto wetu wako barabarani.”

Spika Ndugai ameongeza kwamba “Haiwezekani hata kidogo, kwa hiyo kina mama wale inabidi tufanye utaratibu tujue nini tutafanya lakini pia kuna kina baba wamejitokeza huko nimesikia na baadhi ya walalamikiwa ni kina mama wabunge, kwa hiyo hili jambo halina upande. Hawa kina mama kama wapo, basi waje kwa spika au wamwandikie spika lakini waniletee na DNA test certificate (cheti cha uthibitisho cha vipimo vya vinasaba) ili tuone namna gani ya kuwezesha.

Pamoja na hayo amesema kwamba yapo mafungu ambayo yamepitishwa hivyo wanaweza kuangalia namna ya kuweka sawasawa jambo hilo wabunge wawe na utulivu katika kufanya kazi za Bunge na si kuwa na mawazo mengine.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ametenga siku tano za kuwapa msaada wa kisheria kina mama ambao wametelekezewa watoto na wanaume zao ambapo jana mbele ya Makamu wa Rais Bi. Samia Suluhu alisema kati ya wanawake 480 waliosikilizwa 47 walidai wametelekezewa watoto na wabunge.
Spika ataka DNA za waliozaa na Wabunge Spika ataka DNA za waliozaa na Wabunge Reviewed by Zero Degree on 4/11/2018 12:45:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.