Mahakama yaiagiza TFF kupitia upya suala la Wambura
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura |
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imekubali maombi yaliyopelekwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura ya kutaka kurudia maamuzi ya kamati hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na wakili wake, Emmanuel Muga, hukumu kwenye shauri No.20/2018 iliyotolewa Mei 18, mwaka huu na Jaji Wilfred Ndyasobera baada ya kuridhika na hoja zilizotolewa na mawakili wa Wambura, Dr Masumbuko Lamwai na Muga.
Maamuzi hayo, yanatokana na maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu wiki mbili zilizopita yakiomba mahakama imruhusu Wambura afungue kesi ya msingi kuomba kutengua maamuzi ya kamati ya TFF.
Mahakama imetamka kuwa Wambura kesi yake ina msingi na inafaa isikilizwe. Mahakama imeridhika kuwa maombi yaliletwa ndani ya muda na Wambura ana maslahi mapana ya kuleta maombi, hivyo mahakama imempa ruhusa ya kuleta kesi ya msingi ya kuomba kutenguliwa kwa maamuzi ya kamati za TFF.
Kwa mujibu wa Muga, Mahakama imeamuru kuwa kesi ya msingi ifunguliwe ndani ya siku 14 kuanzia jana. Maombi ya mapitio yaani ‘Judicial Review’ ni haki ya msingi inayotafutwa pale chombo kilichotoa maamuzi kilivunja sheria au kukiuka misingi ya haki kama haki ya kusikilizwa.
“Tunaamini hii haitachukuliwa kama Wambura amepeleka mpira mahakamani, kwani, hii ni ‘judicial review’ ya maamuzi ambayo yalivunja sheria ya TFF wenyewe, pia hayakufuata misingi ya haki ya kusikilizwa.
“Mahakama ipo kwa mujibu wa sheria za nchi, na TFF inafuata sheria hizo, ndiyo maana wamesajiliwa kwa sheria za BMT, na pia waliapishwa na msajili wa vyama vya michezo kwa mujibu wa sheria hiyo,” alisema Muga ambaye amewahi kuwa mwandishi wa michezo wa BBC.
Mahakama yaiagiza TFF kupitia upya suala la Wambura
Reviewed by Zero Degree
on
5/19/2018 08:20:00 AM
Rating: