Loading...

Malinzi, Wambura wapambana Kortini Kisutu

Aiyekuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na watuhumiwa wenzake wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
OFISA Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anapokea mshahara wa Shilingi Milioni 7 kwa mwezi.


Wambura ameyaeleza hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aiyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Shahidi huyo alikuwa akiongozwa na wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake ambapo Wambura alisema aliwahi kuwasilisha maombi ya kutaka kuongezwa mshahara kutoka Shilingi Milioni 2 hadi 7 wakati wa utawala wa Malinzi.

Alipoulizwa na wakili, Rweyongeza kwamba Malinzi alikataa kumuongeza mshahara, Wambura alidai kuwa si kweli, lakini alipeleka maombi hayo tena wakati wa utawala wa Rais wa sasa wa TFF, Walles Karia ambapo aliidhinisha alipwe Sh.Mil 7 tangu Agosti 2017 hadi sasa.

Awali akiongozwa na Wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, Wambura alidai kuwa muhtasari wa June 5, 2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za Benki za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizopo Stanbic ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.

Wambura amedai anasema hayo kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha June 5, 2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.

Baada ya kueleza hayo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 28 na 29, 2018 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa Ofisi wa (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya.
Malinzi, Wambura wapambana Kortini Kisutu Malinzi, Wambura wapambana Kortini Kisutu Reviewed by Zero Degree on 5/22/2018 09:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.