Loading...

Mwanachama Simba SC ajiua


MWANACHAMA wa tawi la Simba Damu Fans (SDF) Tabata Kimanga, Steven Mwashilindi, amejiua kwa kujichoma na kitu chenye ncha kali kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kabla ya mwanachama huyo kujiua, inadaiwa kwanza alimjeruhi mkewe, Maida Mwashilindi, ambaye kwa sasa amelazwa katika wodi ya Kibasila namba 12 katika Hospitali ya Muhimbili, baada ya kutokea kutoelewana kuhusiana na masuala ya kifamilia.

Tukio hilo likitokea Tabata Kimanga, Dar es Salaam, alikokuwa akiishi marehemu na familia yake, ambako inadaiwa mke na mume hao hawakuwa katika maelewano mazuri.

Taarifa kutoka kwa majirani zinadai kuwa, wawili hao walikuwa hawana maelewano, ugomvi huo ulichangiwa na wivu wa kimapenzi, ambao mume alimhisi mkewe kuwa na mahusiano na mtu mwingine, hali iliyopelekea wawili hao kutengana.

“Sakata lilianza Jumamosi, mume alikuwa anahamisha baadhi ya vitu vyake, ilidaiwa kuwa anahama baada ya kodi yake kwisha na mbali na kuhamisha aliamua kuuza baadhi ya vitu.

“Sakata hilo lilianza Jumamosi wakati marehemu alipoonekana kuhamisha vyombo katika nyumba waliyokuwa wakiishi, akidai kwamba amemaliza kodi yake na hivyo anaamua kuhama.

Mke, ambaye kipindi hicho alirudi nyumbani kwao, alipata taarifa kutoka kwa majirani, ndipo aliambatana na kaka yake kwenda nyumbani ili kufanya mazungumzo na mumewe na alipofika walishindwa kuelewana, ndipo mume alipoamua kumjeruhi mkewe.

“Majirani tulishtushwa na kelele za kuomba msaada, tulipoingia chumbani tulimkuta mama yule amejeruhiwa vibaya, ndipo juhudi za kumkimbiza katika Hospitali ya Amana zilipofanywa na baadaye akahamishiwa Muhimbili ambako ndiko alikolazwa hadi muda huu.”

Mtoa habari huyo aliongeza kwamba, mume baada ya kudhani amemsababishia kifo mke wake, naye aliamua kujimaliza kwa kujichoma na kitu hicho chenye ncha kali na kupoteza maisha.

Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tabata Shule na ndugu wa marehemu Steven wanaoishi Tabata Salanga, Kinyerezi, walianza taratibu nyingine zikiwamo za kusafirisha mwili kwa ajili ya mazishi.

Hatimaye mwili wa marehemu uliagwa jana katika Hospitali ya Amana, Ilala na baadaye kusafirishwa kwa maziko katika Mkoa wa Songwe.

Wakati wa ibada fupi ya kuaga mwili, Mzee wa Kanisa la KLPT Kongowe, Karume Ndobho, aliwaasa waombolezaji kutomhukumu marehemu kwa alichokifanya, bali wazidi kumuombea na kuendelea kujifunza kutokana na matendo yake.

Naye mjomba wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Morison Tozo, alisema taratibu zote za Kipolisi walizifuata na kuweza kukabidhiwa mwili kwa ajili ya mazishi.

“Polisi walitutaka tuwataarifu tukishachukua mwili na tulifanya hivyo, awali walituambia kama tuna mashaka na kifo tuwaandikie barua kuwaeleza.

“Tuliwaandikia barua kuwa tunaomba watupe mwili na hatuna mashaka na kifo chake na walitukabidhi,” alisema Tozo.

Marehemu ambaye alikuwa dereva wa bodaboda, ameacha mke na watoto watatu, Mirka Steven, Asiya Steven na Ana Steven.

Mwili wa Steven utazikwa leo mkoani Songwe. Dimba Jumatano lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamdu, ambaye alidai kwamba hakuwa na taarifa hizo kwa vile alikuwa nje ya ofisi kikazi.

Source: Dimba
Mwanachama Simba SC ajiua Mwanachama Simba SC ajiua Reviewed by Zero Degree on 10/17/2018 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.