Loading...

NMB yapunguza tozo akaunti binafsi


BENKI ya NMB imeondoa tozo kadhaa kuanzia Februari Mosi mwaka huu ikiwemo sh 1900/- iliyokuwa ikitozwa kila mwezi kwa ajili ya gharama za ufundi za kibenki.

Mkuu wa Kitengo cha Malipo ya Wateja NMB, Michael Mungure amewaeleza waandishi wa habari kuwa, tozo nyingine iliyoondolewa ni ile ya kufufua akaunti mfu.

Awali kufufua akaunti iliyokaa muda mrefu bila kutumika ilikua inatozwa shilingi 2200 na kama haijatumika mwaka mzima mteja angelazimika kuifufua kwa shilingi 26,400.

Mungure ameitaja tozo nyingine iliyondolewa ni ile ya uhamisho wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine, kwa mfano kuhamisha mishahara, kufanya huduma za kibenki kwa njia ya simu, na kuuliza salio.

Awali huduma hizo zilikuwa zikichajiwa shilingi 800 kwa kila moja. Meneja Mwandamizi Huduma ya Amana NMb, Steven Adil amesema, wameondoa tuzo hizo baada ya utafiti uliofanywa na taasisi za kimataifa uliobainisha kuwa, Watanzania wengi hawatumii huduma za kibenki kutokana na utitiri wa makato.

Amesema pia lengo la kuondoa tozo hizo ni kupata wateja wengi zaidi wa kufungua akaunti katika benki hiyo.

Kwa mujibu wa Adil, akaunti zilizondolewa makato ni zile za binafsi, akaunti za vikundi na fanikiwa, na kwamba, akaunti za kampuni makato bado yanaendelea kama kawaida. Mkuu wa Kitengo cha Wateja, Abella Tarimo amesema, NMB wanaendelea kuboresha huduma kwa njia ya kidijitali kwa gharama nafuu.

Amesema kwa sasa mteja anaweza kufungua akaunti kupitia simu ya mkononi.

“Pia bidhaa yetu ya Klik App, itakuwezesha kufanya miamala mbalimbali kutuma pesa, kulipa deni, kuomba mkopo, kulipia na huduma nyingine,”amesema Tarimo.

Amesema NMB imejipanga kumfikia kila Mtanzania na kumuingiza kwenye uchumi rasmi.

“Kwa kuwa na teknolojia ya kidijitali tuna fursa nzuri ya kuendeleza huduma zetu za mtandaoni katika matawi yetu lengo letu ni kuwapa wateja wetu mamlaka ya kutuma maombi kwa haraka na kwa usalama kwa njia ya kidijitali na kuwapa ushauri kupitia kwa mameneja uhusiano wetu,” amesema.

Tarimo amesema uwezo wa kufungua akaunti mtandaoni ni hatua ya kwanza na wataendelea kuongeza bidhaa nyingine kwa kuzingatia usalama wa fedha za wateja.

Alisema ili mteja aweze kufungua akaunti kupitia simu ya mkononi atatakiwa kubonyeza *150*66# na kufuata maelekezo na ndani ya dakika tatu atapatiwa namba ya akaunti ya simu yake.

“Unaweza kumfungulia mfanyakazi wako akaunti akawa anapata mshahara wake kupitia simu yake ya mkononi, hapa tumemrahisishia muda wa kwenda benki kufungua akaunti pamoja na kujaza fomu nyingi ili apate akaunti,” amesema Tarimo.
NMB yapunguza tozo akaunti binafsi NMB yapunguza tozo akaunti binafsi Reviewed by Zero Degree on 1/30/2019 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.