Ripoti maalum walaji wa nyama Dodoma hatarini
Umaarufu wake, kupendwa kwake katika milo ya kaya za aina zote jijini humo, husababisha mahitaji ya kitoweo cha nyama kuwa juu siku zote.
Hali hiyo imevutia wajasiriamali wengi ambao wamewekeza katika biashara hiyo kwa kujua soko ni la uhakika.
Hata hivyo, changamoto iliyoibuka hivi karibuni ni kuibuka kwa uchinjaji holela wa mifugo, huku wafanyabiashara wa nyama wakidai kuwa hali hiyo inachangiwa na gharama kubwa za kuchinja zinazotozwa na TMC.
Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika mwezi uliopita, ukihusisha ziara kwenye machinjio na maduka ya nyama, umebaini kuwapo kwa changamoto ya uchinjaji holela wa mifugo jijini humo kunakohatarisha afya za walaji wa kitoweo hicho.
Licha ya jiji hilo kuwa na machinjio ya kisasa ya TMC yaliyoko Kizota mjini Dodoma, Nipashe imebaini baadhi ya wafanyabiashara hawapeleki mifugo yao kuchinjwa kwenye machinjio hayo kutokana na kile walichodai kuwa ni gharama kubwa wanazotozwa na kampuni hiyo.
Iddi Kijiko, mfanyabiashara wa nyama, alisema wanalazimika kukwepa kupeleka mifugo yao kuchinjwa kwenye machinjio ya TMC kutokana na gharama kubwa zinazoanzia Sh. 32,500 kwa kila ng'ombe.
“Tunashauri Jiji la Dodoma litafute machinjio yake ili watu wote wakachinje huko, zile nyama zinazochinjwa nje ya TMC ziwe zinakaguliwa na madaktari kama wanaochinja machinjio ya TMC na mnada wa Msalato," alisema.
Kijiko alidai gharama za uendeshaji zinasababisha nyama kilo moja kuuzwa Sh. 6,000 hadi 7,000, kutokana na tozo kubwa zinazolipwa kwa mamlaka, hivyo kuna haja jiji kuchukua hatua.
Selemani Maneno, muuzaji wa nyama, aliwaomba wafanyabiashara wa nyama kuunda umoja ambao viongozi wake watakwenda kuiomba serikali kupunguza ushuru katika machinjio ya TMC.
“Wengi wanachinja machinjio ya mnadani Msalato, wengine porini, inakuwa ni hatari kwa walaji. Ushauri wangu tuwe na machinjio ambayo yatawanufaisha wafanyabiashara na serikali na kuondokana na uchinjaji holela," alisema.
Mkazi wa Dodoma, Eligius Guta, aliziomba mamlaka kufuatilia na kuzuia uchinjaji holela wa mifugo kwa kuwa kuna nyama inauzwa kwa wananchi bila kupimwa, hivyo kuhatarisha afya za walaji.
Hoja hiyo iliungwa mkono na mkazi mwingine wa Dodoma, Rehema Said, ambaye pia aliziomba mamlaka zinazosimamia nyama, kuhakikisha zinafanya ukaguzi ili kuwabaini wanaokiuka taratibu.
“Kuna duka la nyama liko kule Nkuhungu, linauza nyama Sh. 5,000 wakati wengine ni Sh. 6,000, sasa najiuliza, huyu anayeuza bei hiyo anatoa wapi? Nimejaribu kufuatilia inasemekana yeye anachinja mwenyewe huko maporini, kuna haja ya serikali kuchukua hatua maana hali hii ni hatari kwa afya zetu sisi walaji," alisema.
NG'OMBE WAPUNGUA TMC
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TMC (Luziga), alisema tangu kumalizika kwa Operesheni Nzagamba, kumekuwa na uhaba mkubwa wa wateja wanaopeleka mifugo yao kuchinjiwa kwenye machinjio hayo licha ya walaji wa nyama kuongezeka jijini Dodoma.
Alisema kuwa awali kwa siku za kawaida, walikuwa wanachinja ng’ombe 150, lakini kwa sasa wanachinjwa ng’ombe 70 na kwa siku. Luziga alisema kwa siku za mwishoni mwa wiki, idadi ya ng’ombe wanaochinjwa imepungua kutoka 250 hadi 70 kwa siku.
“Huenda mifugo mingi inachinjiwa katika minada ya jirani, kampuni inaathirika kimapato maana mapato makubwa sana yanatokana na huduma ya uchinjaji. Kwa hiyo, utakuta kwamba nusu ya mapato yaliyotarajiwa kukusanywa hayakusanywi," alisema.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa machinjio hiyo yalijengwa mwaka 2002 kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Dola za Marekani milioni 2.6 (Sh. bilioni 6.017).
Luziga alisema makubaliano ya mkataba wa mkopo huo yana kipengele kinachoitaka TMC kuanza kuurejesha baada ya miaka 10 tangu kutolewa kwake (yaani kuanzia mwaka 2012) na inatakiwa kuwa imelikamilisha kuulipa baada ya miaka 50.
“Kutokana na mapato kupungua, inakuwa na madhara, kwa kuwa serikali haipati fedha inayotarajiwa ili kurejesha mkopo," alisema.
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa mamlaka zinazowajibika kusimamia usafirishaji wa mifugo na usalama wa walaji, kuchukua hatua ili kudhibiti uchinjaji holela wa mifugo jijini Dodoma.
KAULI YA WIZARA
Daktari Msimamizi wa Machinjio ya TMC kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mariki Meljory, alisema machinjio ya TMC kwa kiasi kikubwa yanategemewa kwa uzalishaji wa nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa ajili ya soko la ndani jijini Dodoma.
“Siku za karibuni, uchinjaji umeonekana kushuka sana licha ya mahitaji ya soko la nyama Dodoma kuongezeka kwa kiasi kikubwa, inaashiria kuna uchinjaji unaendelea kwenye machinjio yasiyo rasmi," alisema.
Dk. Meljory alisema serikali ilijenga machinjio hayo na kusomesha wataalamu mbalimbali ili kutambua magonjwa na kuhakikisha nyama inayoingia sokoni ni salama na bora kwa walaji.
“Kama kuna uchinjaji unafanyika sehemu ambazo siyo rasmi kwenye minada na nje ya minada, kunaweza kusababisha madhara kwa walaji wa nyama kwa sababu asilimia 70 ya magonjwa yanayowapata binadamu yanatokana na wanyama na mazao ya wanyama," alisema na kuongeza:
“Nyama inapochinjwa na kukaguliwa vizuri, watu wanakuwa wamepunguziwa magonjwa kwa kiasi kikubwa, na kuisaidia serikali kuepuka gharama kubwa kutibu wananchi.
"Kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa ufanisi, katika machinjio haya serikali imeweka wataalamu 13 ambao wamesomea kazi hii."
Dk. Meljory alisema wanyama wanaoingia kwenye machinjio hayo wamekuwa wakikaguliwa vizuri na kunapotokea kuna viashiria vya ugonjwa, mifugo husika haiingii sokoni.
“Sasa, kwa wanaochinjia porini, ni vigumu kutambua kama mnyama ana viashiria vya ugonjwa na matokeo yake inaingia sokoni na ni rahisi kusababisha magonjwa," alisema.
“Wadau mbalimbali wa sekta hii tufuate sheria zilizowekwa na serikali na kwa wale wanaochinja maeneo yasiyo rasmi, watambue wanahatarisha afya za walaji maana wanachinja kwenye maeneo anbako hakuna wataalamu wa kukagua nyama.
"Natoa wito kwa wananchi kupeleka mifugo kwenye machinjio ya TMC yenye wataalamu wa afya ili kupata nyama safi na bora."
Chanzo: Nipashe
Ripoti maalum walaji wa nyama Dodoma hatarini
Reviewed by Zero Degree
on
2/11/2019 08:50:00 AM
Rating: