Loading...

Ulevi wamtia kifungoni muuguzi Arusha


BARAZA la Uuguzi na Ukunga limemsimamisha kazi kwa mwaka mmoja, Muuguzi Martin Chama wa Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha, kwa kosa la ulevi na kushindwa kutoa huduma kwa weledi.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa, ilieleza kuwa mtumishi huyo alitiwa hatiani kwa makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa mbele ya baraza. 

“Kikao cha 196 cha baraza kimeamua kumsimamisha kazi muuguzi Martin Chama kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Februari 7, mwaka huu, baada ya kumtia hatiani na makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa kwenye baraza mwaka jana,” Mtawa alieleza katika taarifa yake hiyo.

Alisema makosa aliyokutwa nayo ni pamoja na kufika kazini akiwa amelewa na kutaka kuhatarisha usalama wa wagonjwa na ndugu zao kwa kushindwa kutoa huduma kwa umakini na weledi.

Mtawa alisema kuwa, awali baraza lilipokea tuhuma kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mount Meru Arusha, kupitia kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni msimamizi wa maadili wa mkoa kwa mujibu wa sheria.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, muuguzi huyo alifika kazini Septemba 26, mwaka jana saa 3:00 usiku akiwa amelewa na alianza kuwasumbua ndugu waliokuwa wakiwaangalia wagonjwa wao kutaka kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa, hali ambayo ingesababisha kuhatarisha maisha ya wagonjwa kwa kuwa hakuwa na umakini,” alisema Mtawa.

Aliongeza kuwa, tuhuma hizo ziliwasilishwa na walalamikaji wawili waliokuwa wakiuguza wagonjwa wao.
Mtawa alisema walianza kufanya uchunguzi wa awali na kubaini upungufu uliofanywa na muuguzi huyo ambao ni kinyume cha maadili ya uuguzi na ukunga.

“Taarifa hii ilipelekwa katika kikao cha dharura cha bodi cha 195 ambacho pamoja na mambo mengine, kilijadili na kuamua shauri hili lisikilizwe kataka kikao cha bodi cha 196 ambayo itahusisha mtuhumiwa na mashahidi ambao ni walalamikaji na watumishi waliokuwapo na kutoa hukumu hiyo,” alisema Mtawa.

Alisema baraza hilo lilianzishwa ili kulinda umma kutokana na huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini na linafanya kazi kwa kusimamia ubora katika mafunzo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vilivyowekwa.
Ulevi wamtia kifungoni muuguzi Arusha Ulevi wamtia kifungoni muuguzi Arusha Reviewed by Zero Degree on 2/11/2019 07:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.