Yanga yaing'oa Biashara United Kombe la FA
YANGA, jana Alhamisi iliibuka na ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Biashara United na kufanikiwa kufuzu Hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA.
Ushindi wa Yanga umekuja baada ya dakika 90 za mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mchezo ulianza kwa kasi na dakika ya kwanza tu, Biashara United walizawadiwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ kumchezea vibaya, George Makang’a na Waziri Junior akafunga bao la kwanza dakika ya tatu.
Baada ya kuingia kwa bao hilo la mapema, Yanga wakaamka na dakika ya saba, nahodha wa kikosi hicho, Ibrahim Ajibu, akaangushwa kwenye eneo la hatari, Amissi Tambwe akafunga kwa penalti dakika ya tisa.
Biashara United wakazichanga vizuri karata zao, dakika ya 40 wakaongeza bao la pili kupitia kwa Innocent Edwin ambaye kwanza alimpunguza Kelvin Yondani kabla ya kuuzungusha mpira na kumuacha Ramadhan Kabwili akishindwa kudaka. Hadi mapumziko, Biashara United ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga ilisubiri mpaka dakika ya 73 kusawazisha bao hilo kupitia kwa Heritier Makambo kutokana na walinzi wa Biashara United kujichanganya.
Tukio la kushangaza katika mchezo huo lilitokea dakika ya 83 baada ya kipa wa Biashara United, Nurdin Bazora, kugombana na kocha wake, Amri Said ikiwa ni muda mfupi baada ya kufanyiwa mabadiliko, ambapo mabishano hayo yalimfanya mwamuzi, Martin Saanya kumuondoa kipa huyo na kwenda vyumbani.
Katika mikwaju ya penalti, Yanga walifunga zote kupitia kwa Heritier Makambo, Paul Godfrey, Ibrahim Ajibu, Thaban Kamusoko na Matheo Anthony.
Upande wa Biashara United, penalti zao zilifungwa na Lenny Kissu, George Makang’a, Derrick Mussa na Kauswa Bernard, huku Tariq Seif akikosa.
Kwa ushindi huo, sasa Yanga itacheza na Namungo katika Hatua ya 16 Bora ya Kombe la FA dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo mkoani Lindi ambapo mechi za hatua hiyo zitachezwa kati ya Februari 22 na 25, mwaka huu.
Yanga yaing'oa Biashara United Kombe la FA
Reviewed by Zero Degree
on
2/01/2019 07:20:00 AM
Rating: