Loading...

JPM: Inaumiza sana tunapopewa madaraka halafu tunajisahau


MAAGIZO ya Rais John Magufuli kwa watendaji wake yamekuwa pasua kichwa, baada ya kuagiza utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa ufukwe wa Coco Beach ndani ya mwezi mmoja mara mbili na kuonekana utekelezaji wake ni ndivyo sivyo, Manispaa imepata kigugumizi kuzungumzia hilo.

Wiki moja iliyopita, Rais Magufuli alionyesha kukerwa na baadhi ya viongozi ambao hawasimamii na kuchukua maamuzi utekelezaji wa miradi ya maendeleo ukiwamo uendelezaji wa ufukwe wa Coco.

Baada ya kauli hiyo siku iliyofuata viongozi wa Manispaa ya Kinondoni waliibukia Coco na kutangaza kufunga kupisha ujenzi.

Juzi, Rais Magufuli wakati akiwaapisha baadhi ya viongozi aliowateua Ikulu jijini Dar es Salaam miongoni mwa mambo aliyoyazunguzia ni ujenzi wa ufukwe huo na kushangaa mkandarasi kukabidhiwa Sh. bilioni 14 kwa ajili ya kujenga ghorofa moja.

Rais Magufuli alisema eneo ambalo mkandarasi amekabidhiwa kwa ajili ya ujenzi huo ndipo patajengwa mradi wa ujenzi wa daraja jipya la Selander, litakaloanzia ufukwe wa Coco Beach (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan.

Hata hivyo, jana Nipashe ilipomtafuta Mkurugenzi wa Manispaa, Aron Kagurumjuli, ili kujua nini kinachoendelea baada ya maagizo ya Rais, alijibu kwa kifupi: “Siwezi kuyajadili maagizo ya Rais.”

Juzi, Rais Magufuli alisema mkandarasi alipopewa zabuni ya kujenga eneo hilo ndiye aliyeshindwa kujenga soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya.

“Sasa sijui wakishajenga hiyo ghorofa lao, halafu ujenzi wa barabara nne utakapoanza sijui watalibomoa hilo jengo lao?” Zitapita wapi?” Unapojenga wachuuzi wa eneo lile watakwenda wapi?” Wata survive (kuishi) namna gani?” Alihoji Rais na kuongeza:

“Inaumiza sana tunapopewa madaraka halafu tunajisahau, Coco Beach haiwezi kujengwa kwa Sh. bilioni 14, unajenga lighorofa la nini?” Nendeni beach (fukwe) zingine mkaone zinavyojengwa.”

Akizindua kiwanda cha kutengeneza mabomba Vingunguti jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Magufuli alionyesha kukerwa na baadhi ya viongozi ambao hawasimamii na kuchukua maamuzi utekelezaji wa miradi ya maendeleo ukiwamo uendelezaji wa ufukwe huo.

Alisema baadhi ya miradi inayocheleweshwa ni kiwanda cha machinjio Vingunguti na ufukwe wa Coco.

Baada ya kauli hiyo, kesho yake, Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta, akiwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Kagurumjuli, walifika kwenye ufukwe huo na kutangaza rasmi kuwa Coco kunafungwa kwa muda kupisha ujenzi uliolenga kupaendeleza ili uwe wa kisasa.

Sitta aliwaeleza wanahabari kuwa ufukwe huo umefungwa kwa muda kupisha ujenzi ambao utachukua miezi sita kuanzia sasa na utagharimu Sh. bilioni 13.6.

“Tutafunga mpaka kule wanakouza mihogo, wanaouza mihogo wameshapewa notisi ili watafute sehemu nyingine, tutafunga eneo hili lote kwa mabati ili makandarasi wafanye kazi bila kuleta matatizo, mkiona ufukwe umefungwa ni kwa maslahi mapana manispaa na mkoa wetu,” alisema.

Alisema awali waliomba Sh. bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi huo lakini baada ya mazungumzo na mkandarasi imeshuka hadi Sh. bilioni 13.6.

“Ninaishukuru timu ya wataalamu na makandarasi wameonyesha uzalendo, tutahakikisha tunapata ufukwe wa kimataifa ili watu wakija kupumzika wapate madhari kama ya Afrika Kusini au Uingereza na kwingine,” alisema.

Alisema mradi huo ni wa pili ambao Manispaa inautekeleza sambamba na ujenzi wa soko la Tandale ambapo taratibu za kisheria zote zimefuatwa.

Kagurumjuli, alisema kwa upande wa manunuzi hawakuruka hata kipengele kimoja, hivyo kwenye eneo hilo wapo salama.

Alisema mkandarasi anayeliendeleza eneo hilo ataifanya shughuli hiyo kwa miezi sita na kuikabidhi.

Chanzo: Nipashe
JPM: Inaumiza sana tunapopewa madaraka halafu tunajisahau JPM: Inaumiza sana tunapopewa madaraka halafu tunajisahau Reviewed by Zero Degree on 9/24/2019 08:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.