Loading...

Rais ataja sababu za kumtumbua Mkuu wa Mkoa wa Morogoro


RAIS John Magufuli amesema sababu iliyomsukuma kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, ni utendaji mbovu wa kiongozi huyo katika kusimamia majukumu yake.


Alisema Mkuu huyo wa Mkoa alishindwa kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na watendaji waliochini yake kufanya kazi chini ya kiwango.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa, makatibu wakuu na manaibu katibu mkuu, Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Ukishaona RC (Mkuu wa Mkoa) yupo pale automatically ameshindwa kuhimili mkoa wake, ukishaona DC (Mkuu wa Wilaya) na DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) wanagombana kisa maslahi, na Mkuu wa Mkoa hujawahi hata kufika kukemea maana yake hatoshi,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Mkoa wa Morogoro ulitusumbua sana katika kuongoza, mambo mengi yalikuwa hayaendi, nisipoyasema hapa nitakuwa mnafiki, na mimi sitaki kuwa mnafiki, ukienda kwenye halmashauri utakuta matumizi ya pesa ya ovyo, kila unapogusa ni ovyo tu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu sana, na kwamba kazi inayompa shida ni ya mtu anayemteua kisha anamtengua, alisema ni kazi yenye machungu.

“Haiwezekani watendaji waliochini yako hawafanyi vizuri halafu unajiita RC (Mkuu wa Mkoa) ndiyo maana nikampeleka huyu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, ninajua nampeleka mahali kwenye changamoto nyingi, na ni mtego kwake,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi Morogoro kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, lakini havikamiliki, alisema migogoro ya ardhi ipo kila mahali.

Rais Magufuli alisema hata wawekezaji wa tumbaku mkoani Morogoro wanataka kukimbia na kiwanda kukifunga.

“Wewe (Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mpya) kwa kuwa umetoka Arusha na unawajua vizuri wafugaji, nimekupeleka Morogoro ili ukatatue changamoto za wakulima na wafugaji, usimwonee mtu, miradi haiendi Sh. bilioni 1.3 tumepeleka za ujenzi wa zahanati mwezi mzima hazijatumika,” alisema.

Rais alisema Mkoa wa Morogoro ulipaswa kucholewa demo kwa kuwafukuza viongozi wote wa serikali kuanzia Mkuu wa Mkoa hadi kiongozi wa chini kwa siku moja, kisha kuwateua wengine.

Aidha, Rais Magufuli alisema yeye huwa hatengui kiongozi yeyote bali wanajitengua wenyewe, na kwamba ukiona anatengua kiongozi huyo ameshindikana.

“Kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu, kuna siku nilikuwa na Katibu Mkuu Kiongozi tulikaa hadi usiku, nikamwambia nimechoka kichwa kinaniuma ngoja nikalale, nikaenda kulala nikamwacha, niliporudi na yeye sikumkuta. Unayemtengua hujui ana mapepo kiasi gani, wala ana malaika kiasi gani,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema kuna muda alilazimika kumtumia meseji Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kumweleza ashughulikie suala fulani, alikuwa anajibiwa litafanyika, lakini lilikuwa halifanyiki.

Chanzo: Nipashe
Rais ataja sababu za kumtumbua Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Rais ataja sababu za kumtumbua Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Reviewed by Zero Degree on 9/23/2019 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.