Loading...

Siku 14 zatolewa kwa wazalishaji wa mifuko mbadala


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene, ametoa siku 14 kwa watengenezaji na wasambazaji mifuko mbadala hapa nchini kuhakikisha inakidhi vigezo vyote stahiki, ikiwemo uwekaji nembo ya mmiliki au kampuni.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam baada ya kufanya ziara Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema kuwa uwepo wa wazalishaji wa mifuko mbadala ambao hawakidhi vigezo na masharti yaliyowekwa na mamlaka husika, inasababisha wazalishaji wa ndani kukosa soko na kupoteza mapato ya Serikali.

“Ni lazima tujue nani anazalisha na kusambaza mifuko hii mbadala, hawa wanaozalisha ndani na kufuata taratibu zote wanakosa soko kwa sababu ya wengine wanaofanya biashara hii kiholela bila kufuata taratibu,” alisema Simbachawene.

Mbali ya agizo hilo, alisema baada ya muda kufika msako mkali utafanyika na kwa yeyote atakayekutwa akizalisha au kuuza mifuko mbadala isiyofikia vigezo vilivyowekwa na mamlaka husika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, ikiwemo pia kuchomwa kwa mifuko hiyo.

Aidha Simbachawene aliagiza watumishi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kitengo cha ukaguzi bandarini kufanya kazi saa 24 wakishirikiana na watumishi kutoka taasisi nyingine za Serikali ili kuongeza nguvu kazi katika suala zima la ukaguzi wa mizigo inayoingia nchini.

“Ufanisi wa bandari upo kwenye utoaji na uingizaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Ikibidi nguvu kazi iongezeke ili kazi hii ifanyike kwa haraka na uhakika,” alisema.

Aliongeza kuwa kanuni zimebainisha wazi kuwa mtu yeyote anayeingiza nchini, anayesafirisha nje ya nchi au anayezalisha vifungashio vya plastiki ambavyo havijazuiwa na kanuni hizi, anatakiwa kuhakikisha kwamba vinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Tupo vizuri na tumejipanga kuhakikisha kuwa biashara hizi za ujanja ujanja zinatokomezwa. Wakati umefika kwa Watanzania kufanya kazi halali na kuzingatia sheria,” alisema.

Tangu Serikali iweke katazo la utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki Juni mwaka huu, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha mifuko mbadala inatumika na kusaidia kuiweka Tanzania kuwa sehemu salama katika utunzaji wa mazingira.
Siku 14 zatolewa kwa wazalishaji wa mifuko mbadala Siku 14 zatolewa kwa wazalishaji wa mifuko mbadala Reviewed by Zero Degree on 9/26/2019 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.