Loading...

Bado hatujamaliza msimu - Gamondi


Licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu huku wakiwa na michezo mitatu mkononi, Kocha wa Yanga, Miguel gamondi, amesema kwake bado hawajafikia malengo yao msimu huu mpaka watakapotwaa ubingwa wa kombe la FA.

Kocha huyo amewataka wachezaji wake kukumbuka mipango yao tangu walipoanza msimu.

Gamondi amesema wanatakiwa kuendelea kupambana na kutwaa ubingwa wa kombe la FA ili kutimiza malengo waliyojiwekea tangu kuanza kwa msimu huu wa 2023/2024.

“Bado hatujamaliza msimu, tulikuwa na michuano mitatu, Ligi ya mabingwa, Ligi Kuu na Kombe la FA, kwangu ingawa katika mashindano mawili tumefanikiwa kufikia malengo, bado nahitaji kuona tunachukua kombe la FA,” alisema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, alisema katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika ingawa walitolewa katika hatua ya robo fainali, walifikia malengo waliyojiwekea kabla ya kuanza michuano hiyo mikubwa Afrika.

“Lengo letu kubwa ilikuwa kucheza hatua ya makundi, tulifanikiwa na kwenda mbali zaidi na kucheza robo fainali, ukirudi kwenye Ligi Kuu hivyo hivyo tumefanikiwa kuchukua ubingwa, ukiangalia hapo sasa tumebakisha kombe la FA ambalo nalo lilikuwa kwenye malengo yetu,” alisema Gamondi.

Kwa sasa Yanga wapo kwenye maandalizi ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu FC (Singida Black Stars) utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Gamondi, alisema tayari wameshaanza maandalizi ya mchezo huo muhimu na kuwataka wachezaji kuweka akili na mawazo yao kwenye mchezo huo.

“Huu hauwezi kuwa mchezo mwepesi, ni mtoano, makosa kidogo yanaweza yakatugharimu na kushindwa kufikia lengo letu, nimeongea na wachezaji na tunaendelea na maandalizi ya mchezo huo,” alisema Gamondi.

Alisema anatamani mechi hiyo iishe ndani ya dakika 90 za mchezo na wachezaji wake wanaweza wakafanya hivyo kama watafuata vizuri maelekezo yake kama wanavyofanyaga siku zote.
Bado hatujamaliza msimu - Gamondi Bado hatujamaliza msimu - Gamondi Reviewed by Zero Degree on 5/17/2024 05:43:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.