Loading...

Mikoa inayoongoza kwa kuwa na mbwa wengi zaidi


Mikoa ya Geita, Mwanza na Tabora inaongoza nchini kwa kuwa na mbwa wengi kwa mujibu wa taarifa ya Sampuli ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2020.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, alibainisha hayo jana bungeni alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Yustina Rahhi aliyetaka kujua idadi ya mbwa nchini.

Mnyeti alisema kuna mbwa 2,776,918 nchini na mikoa iliyoongoza kwa mbwa wengi ni Geita (302,879), Mwanza (287,270) na Tabora (243,768).

Alisema wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuhakikisha takwimu sahihi za mifugo ikiwamo mbwa zinapatikana kwa wakati ili kuwezesha mipango ya serikali ya kuendeleza sekta ya mifugo.

Akiuliza swali la nyongeza, mbunge huyo alisema ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni changamoto kubwa hasa kwa jamii ya wafugaji walioko vijijini na matibabu yake ni shida kwa sababu hayapatikani katika zahanati na vituo vya afya, hivyo takribani Watanzania 1,500 hupoteza maisha kila mwaka.

"Serikali ina mpango gani kudhibiti kichaa cha mbwa nchini? Njia pekee ambayo serikali inatumia kudhibiti mbwa wazururaji ni kuwapiga risasi. Kwanini serikali inakiuka haki za wanyama?" alihoji.

Pia alitaka serikali kufikiria kufanya alichokiita uchumi wa mbwa kutokana na idadi kubwa ya mbwa nchini kwa kuwafundisha na kuwauza ndani na nje ya nchi.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Mnyeti alisema serikali imeshatoa rukhsa wadau mbalimbali kutoa chanjo kupitia sekta binafsi ili kukabiliana na kichaa cha mbwa.

"Dawa ya kwanza ya kichaa cha mbwa ni kumchanja mbwa mwenyewe, tusisubiri mpaka mbwa augue kichaa cha mbwa ndipo achanjwe, kwa sababu anapougua matibabu yake huwa ni muhimu sana.

"Nitoe rai kwa wadau wote kuendelea kuchanja mbwa ili kudhibiti kichaa cha mbwa kwa sababu hakuna mbadala mwingine tofauti na hapo," alisema.

Mnyeti alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha mbwa wote ambao wamo ndani ya nchi wanaendelea kuchanjwa kwa wakati.

Kuhusu mkakati wa kuzuia mbwa wanaozurura mitaani, Mnyeti alisema mbwa anapokuwa ameshaumwa kichaa kumdhibiti ni pamoja na kuchukua hatua ngumu ya kumuua.
Mikoa inayoongoza kwa kuwa na mbwa wengi zaidi Mikoa inayoongoza kwa kuwa na mbwa wengi zaidi Reviewed by Zero Degree on 5/22/2024 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.