Loading...

Kasi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme Jua Kishapu, wamkosha balozi wa Ufaransa


Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania Bi. Anne Sophie Ave ametembelea na kukagua Mradi wa kuzalisha umeme wa Jua (solar) uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na kujionea kasi kubwa ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo ambao mpaka sasa umefikia asilimia 67.

Akizungumza katika ziara hiyo Juni 27,2025 Balozi amesema kuwa dhumuni la ziara hiyo ni kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Tanzania ambayo inafadhiliwa na umoja wa Nchi za ulaya ikiwemo Ufaransa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.

“Sababu kubwa ya mimi kuja hapa, ni kutaka kujionea miradi ya maendeleo ambayo Umoja wa Nchi za Ulaya na Shirika la maendeleo la Ufaransa inaifadhili, ikiwemo mradi huu wa kuzalisha umeme wa jua hapa Kishapu, nimeona tija ya mradi huu kwa wananchi lakini pia nimeona thamani ya pesa ambayo tumeitoa, kazi ni nzuri na watendaji kazi hapa wanafanyakazi kwa bidii na kujitoa sana, niwaombe waendelee kujitoa ili mradi huu ukamilike kwa wakati na watanzania wapate umeme” alisema Balozi Anne.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi Amesema kupitia ufadhili wa Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD)Kiasi cha Shilingi Bilioni 323 kimetumika katika kutekeleza Mradi wa umeme jua utakaozalisha Megawati 150 na kuwataka Watanzania wakae tayari katika kuutumia Umeme huo kwa maendeleo ya uchumi wao na wataifa kwa ujumla.

Naye, Mkurugenzi Wa Miradi TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya Amesema kuwa Umoja wa Nchi za Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) umefadhili miradi mbalimbali ya umeme kupitia Serikali ya Tanzania ikiwemo Mradi wa Kakono, Mradi wa kuinganisha Tanzania na Zambia (TAZA), Mradi wa kuinganisha Tanzania na Uganda na pia imeonesha nia ya kuendelea kuifadhili miradi mingine ya Umeme.

Ameongeza kwa kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya umeme itakayowezesha kuwepo kwa umeme wa uhakika na hivyo kuiwezesha Tanzania kutekeleza mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme.





Kasi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme Jua Kishapu, wamkosha balozi wa Ufaransa Kasi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme Jua Kishapu, wamkosha balozi wa Ufaransa Reviewed by Zero Degree on 6/28/2025 07:07:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.