Loading...

Lowassa: Polisi msitutafutie sababu bure

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa  

Mvutano wa shughuli za kuaga mwili wa Mawazo ulijitokeza baada ya polisi mkoani hapa kupiga marufuku shughuli hiyo kwa madai ya kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu. Hadi sasa mwili huo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC), Mwanza.

Mwanza.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia kuagwa kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo na leo kimepanga kufungua kesi katika Mahakama ya Kuu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, kutaka kupewa ufafanuzi wa suala hilo.

Aidha, aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho Edward Lowassa amesema uchaguzi umemalizika watu waache maneno na vijembe na kwamba polisi wasitafute sababu za kutumia magari ya maji ya kuwasha waliyoyanunua kwa fedha nyingi katika uchaguzi mkuu uliomalizika.
Mvutano wa shughuli za kuaga mwili wa Mawazo ulijitokeza baada ya polisi mkoani hapa kupiga marufuku shughuli hiyo kwa madai ya kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu. Hadi sasa mwili huo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC), Mwanza.

Amri hiyo ya kupiga marufuku ilitolewa Ijumaa na kamanda wa polisi wa mkoa, Charles Mkumbo aliyesema wamezuia mikusanyiko kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Jana Polisi waliondoa uwezekano wa viongozi na wanachama wa Chadema kuuchukua mwili na kufanya taratibu za kuuaga.

Pia, amri nyingine kama hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie lakini yeye akidai Mawazo si kiongozi wa kitaifa wala mkazi wa mjini Geita.


Freeman Mbowe
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza, baada ya kumalizika kwa vikao vya viongozi wakuu wa Chadema, uliofanyika tangu juzi, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe alisema wanatambua polisi wanashinikizwa kufanya hivyo, lakini Mawazo lazima aagwe, kwani ni kiongozi wa kitaifa.

“Tunatambua kwamba polisi wanashinikizwa kufanya wanachokifanya, lakini naomba watambue kwamba Mawazo alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa, alikuwa mwenyekiti wa Chadema Geita, alikuwa mjumbe wa uongozi Kanda ya Ziwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda. Hivyo anastahili kuagwa na kuzikwa kwa heshima zote,” alisema Mbowe.

“Nimefanya mazungumzo na IGP (Ernest Mangu), na sababu alizonieleza kuzuia watu kuaga mwili wa Mawazo siyo za msingi. Tumeshuhudia viongozi mbalimbali wa kitaifa wakifariki wanaagwa, wasanii wanaagwa kwa nini sisi Chadema tusimuage mwenzetu? Kama sababu ni kipindupindu kwanini hawazuii mikusanyiko ya ibada?” alihoji Mbowe.

Mbowe alisema wamekubalina na familia kufungua kesi hiyo ili kuomba ufafanuzi wa mahakama na kwamba wapo tayari kuheshimu maamuzi yatakayotolewa licha ya kwenda Mwanza na ujumbe wa wabunge 45.


Frederick Sumaye

Naye Waziri mkuu mstafu wa awamu ya tatu, Federick Sumaye alisema Tanzania ni nchi ya amani kutokana na misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili, lakini vyombo vya dola vimejipa jukumu la kulinda amani hiyo kwa nguvu.

“Mimi sijawahi kuona Serikali ikikataza watu kuaga mwili wa marehemu. Kama watu walifanya uchaguzi kwa amani, iweje mtu akatazwe kuaga mwili? Kwani wameambiwa watu wanataka kuandamana? Tena walitakiwa kutoa ulinzi watu waage wamalize kwa salama,” alisema Sumaye.

Kauli ya mchungaji.

Mchungaji Charles Lukiko ambaye ni baba mdogo wa Mawazo aliwaambia waandishi wa habari akisema: “Mwanangu aliniambia ‘baba najinyima kuvaa suti, nimeacha kuendelea na masomo ya chuo kikuu na nitakufa kwa kutafuta haki ya Watanzania.

“Kitendo kinachofanywa na polisi ni cha udhalilishaji kwa kuwa tangu juzi polisi wamejaa nyumbani kwangu. Mbaya zaidi watu wakija kwenye maombolezo wanapigwa mabomu kama ilivyotokea juzi. Mama yake aliniambia kwamba akazikwe kijijini kwao tutafanya hivyo, lakini wenzake wana haki ya kumuaga.”


Kifo cha Mawazo

Mawazo aliuawa Novemba 14 baada ya kutekwa na kundi la watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM ambao walimshambulia kwa silaha za jadi. Alikuwa mjini Katoro, Geita kuhudhuria kikao cha ndani cha maandalizi ya uchaguzi mdogo kata ya Ludete.


Vifo vingine


Hii si mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kuzua kuaga mwili wa mfuasi wa upinzani. Juni 7, 2012 Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mkoani Mara, kilitwaa kutoka hospitalini mwili wa marehemu Mgosi Magasi Chacha (30), aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi wanaolinda mgodi wa North Mara.





Lowassa: Polisi msitutafutie sababu bure Lowassa: Polisi msitutafutie sababu bure Reviewed by Zero Degree on 11/23/2015 11:13:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.