Loading...

Kardinali PENGO alazwa muhimbili.



Rais John Magufuli na mkewe Janeth wakimjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Muhimbili, Dar es Salaam.



Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na ugonjwa ambao haujawekwa wazi.

Kardinali Pengo, alipelekwa hospitalini hapo juzi usiku na kulazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Rais John Magufuli jana alikwenda kumuona na ujio wake wa ghafla uliwashtua watumishi wa hospitali hiyo wakidhani amefanya ziara nyingine ya kushtukiza.

“Alivyofika huyu bwana mkubwa (Rais Magufuli) hapa palikuwa ni hekaheka, mara daktari huyu kaenda huku na yule kaenda kule. Maana walijua ujio wake una jambo,” alisema mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Baadaye, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilieleza kuwa Dk Magufuli aliyeambatana na mkewe Janeth,

alimpa pole Kardinali Pengo na kumwombea afya njema ili aweze kuendelea na shughuli zake za kutoa huduma za kiroho.

Taarifa hiyo ilimkariri kaimu mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi akisema afya ya kiongozi huyo wa kidini imeendelea kuimarika ikilinganishwa na alivyofikishwa katika taasisi hiyo juzi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Profesa Janabi hakubainisha tatizo linalomsibu Kardinali Pengo, akisema maadili ya kazi yake hayamruhusu.

Katika mkesha wa Krismasi wiki iliyopita, Kardinali Pengo alionekana hadhariani, akihubiri katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph huku akiwa ameketi na kusema Watanzania wanyonge na maskini, hawatakiwi kuogopa kuonyesha uwezo wao kwa kuwa sasa wana nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko kwa jamii kuliko matajiri.

Alisema zama za kusadikishwa kwamba matajiri pekee ndiyo wenye uwezo wa mkubwa wa kuongoza na kuleta mabadiliko ya kidini, kisiasa na uchumi, zimekwisha.

Oktoba 15, 2014 wakati akihubiri kwenye ibada maalumu ya misa iliyoandaliwa na Utume wa Wanaume Katoliki (Uwaka), Jimbo la Dar es Salaam, Kardinali Pengo alizungumzia afya yake baada ya kutoonekana hadharani kwa muda mrefu kutokana na kuumwa.

Hata hivyo, katika ibada hiyo hakutaja ugonjwa unaomsumbua. Machi mwaka huohuo, akiadhimisha miaka 30 ya uaskofu wake, ilielezwa kuwa alikuwa mgonjwa asiyetakiwa kusafiri umbali mrefu.

“Wapo watu wengi walikuwa wana wasiwasi kuhusu hali yangu, wengine si Wakristo, walinipigia simu kunijulia hali. Nawashukuru wote kwa kuniombea, sasa nimepata nafuu,” alisema.

Aliongeza, “Najua wengi wanashangaa kuona askofu wao akitembea namna hii, kwa mkongojo, hivi ndivyo ilivyo, nilikuwa mgonjwa, lakini nawashukuruni nyote kwa kuniombea, Mwenyezi Mungu awabariki,” Kardinali Pengo alinukuliwa na gazeti hili wakati huo.

Kardinali Pengo ambaye hivi sasa anakaribia miaka 72, katika ibada hiyo alifafanua kwamba, hata kama afya yake isingetetereka, alikuwa amebakiza miaka mitano kustaafu uongozi wa kanisa hilo kulingana na kanuni.

Alisema hakukuwa na sababu ya msingi ya waumini kuanza kuingiwa hofu yoyote kuhusu mrithi wa nafasi yake, kwani kanisa hilo lina mfumo imara wa kuwapata viongozi wake.


Source:Mwananchi


Comment & Share this story!!
Kardinali PENGO alazwa muhimbili. Kardinali PENGO alazwa muhimbili. Reviewed by Zero Degree on 1/02/2016 04:46:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.