SIKU 100 ZA JPM: Matokeo ya utafiti mpya uliofanywa yanaonyesha kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umeongezeka kufikia 74.5%.
Magufuli alishinda mbio za urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, akipata asilimia chache kuliko wagombea wengine kutoka CCM, lakini amejiongezea umaarufu kutokana na hatua ambazo amekuwa akichukua tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015.
Katika uchaguzi huo, Dk Magufuli alipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47, akifuatiwa na Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97.
Lakini utafiti huo uliofanywa na taasisi ya Ms Infotrak Researc and Consultant na Ms Midas Touche East Africa kwa kuwahoji watu 1,200 wenye umri wa zaidi ya miaka 18 katika kanda sita na mikoa 15, unaonyesha kuwa Magufuli ameongeza umaarufu kwa takriban asilimia 20, huku Lowassa akishuka kwa asilimia 20 pia.
Katika utafiti huo, Lowassa anaonekana kushuka hadi asilimia 20.1.
Wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni Anna Mghwira aliyepata asilimia 1.1, Hashimu Rungwe (0.4), Fahmi Dovutwa (0.2), Lutalosa Yemba (0.1), Janken Kasambala (0.1) na Machmillan Lyimo aliyepata asilimia 0.0. Asilimia 3.5 ya walioulizwa swali hilo walikataa kujibu.
Vilevile, wananchi walipouliza iwapo Uchaguzi Mkuu ukifanyika leo wangemchagua nani kati ya makada waliojitokea kugombea urais mwaka jana, wengi wamemtaja Magufuli.
Matokeo hayo yanaonyesha kwamba wanawake wengi ndiyo wanamuunga mkono Magufuli ikilinganishwa na wanaume. Asilimia 77.9 ya wanawake wanasema wapo tayari kumchagua tena kuwa Rais iwapo kutakuwa na uchaguzi mpya, wakati wanaume wanaosema hivyo ni asilimia 71.5 pekee.
Kinyume na ilivyo kwa Magufuli, utafiti umebaini kwamba Lowassa anapendwa zaidi na wanaume huku asilimia 22.6 wakisema wapo tayari kumchagua kuwa rais. Ni asilimia 17.4 ndiyo wametoa maoni kama hayo kwa Magufuli.
Kwa upande wa kanda; Kanda ya Zanzibar ndiyo inayoongoza kwa ‘kumkubali’ Magufuli ikiwa na asilimia 91.6, ikifuatiwa na Kanda ya Kati yenye asilimia 81.6, Kanda ya Kaskazini (77%), Kanda ya Pwani (72.7) na Kanda ya Ziwa asilimia 67.6.
Alipoulizwa kuhusu matokeo ya utafiti huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbuso alisema kuongezeka kwa umaarufu wa Rais Magufuli kunatokana na utendaji wake kugusa kero za wanyonge.
Alisema Watanzania wengi hata wale waliokuwa wakiunga mkono vyama vya upinzani, wameanza kukubaliana na Magufuli kutokana na namna alivyoweza kufanya mambo makubwa na yenye umuhimu kwa Taifa ndani ya muda mfupi.
“Hakuna Rais aliyefanya mambo makubwa namna hii ndani ya siku 100 ndiyo maana wanyonge wameonekana kumkubali kwa sababu amegusa na kuonyesha wazi nia ya kumaliza changamoto zao,” alisema.
“Hata ikitokea uchaguzi ukafanyika sasa nina uhakika Magufuli atashinda kwa sababu wananchi wamebaini wazi kuwa anachokizungumza ndicho anachomaanisha. Si siasa kama ambavyo imezoeleka kwa wanasiasa wengine.”
Maoni yake yanalingana na ya naibu katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Hezron Kaaya aliyesema kasi aliyoanza nayo inaridhisha kiasi cha kuwatia moyo wafanyakazi kuwa huenda kero na changamoto zao zinaelekea kutatuliwa.
“Tucta tulishapigia kelele muda mrefu mambo mengi ambayo Magufuli anayatumbua kwa sasa, mfano suala la ukwepaji kodi na wizi bandarini. Tulishikilia kidete tukiamini kwamba ni mianya ya kulikosesha taifa mapato,” alisema Kaaya.
Kaaya alisisitiza kuwa Magufuli akiendelea na kasi hiyo ni wazi kuwa taifa litasonga mbele na kupata maendeleo ndani ya kipindi kifupi.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa Tanzania Labour Party na mbunge wa zamani wa Vunjo, Augustine Mrema aliyesema kuwa Watanzania walifanya uchaguzi sahihi kumuweka Magufuli madarakani.
Alisema katika kipindi cha siku 100 kiongozi huyo amefanya miujiza ambayo hakuna Mtanzania ambaye alifikiria kuwa ingeweza kufanyika.
“Kwa kazi na makubwa aliyofanya namvulia kofia. Anaonekana wazi ana nia ya kutuondoa kwenye umaskini na dalili tumeshaziona tusubiri makubwa zaidi,” alisema Mrema.
Source: Mwananchi
ZeroDegree.
SIKU 100 ZA JPM: Matokeo ya utafiti mpya uliofanywa yanaonyesha kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umeongezeka kufikia 74.5%.
Reviewed by Zero Degree
on
2/13/2016 11:37:00 AM
Rating: