Loading...

Mwisho wa ‘vilaza’ elimu ya juu rasmi.

Waziri wa Elimu Pro. Joyce Ndalichako.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema sifa za kujiunga na vyuo vikuu na kidato cha tano zimepandishwa ili kuinua kiwango cha elimu ya juu.
Ili mwanafunzi aweze kwenda kidato cha tano sasa, alisema Prof. Ndalichako, ni lazima awe na alama C na kuendelea kwenye masomo mawili kati ya matatu atakayokwenda kusomea.

Kwa vyuo vikuu, alisema Waziri Ndalichako, mwanafunzi atakayetaka kusoma shahada ya kwanza akitokea kwenye stashahada atatakiwa kuwa na GPA ya kuanzia 3.5 huku yule anayetoka kidato cha sita akiwa na alama nne (kuanzia D mbili).

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni takribani miezi saba tangu Prof. Ndalichako atangaze kufuta mfumo wa kutunuku madaraja kwa wahitimu wa kidato cha nne kutoka ule wa wastani za alama (GPA) kwenye jumla ya alama (divisheni).

Akizugumza katika mahojiano maalum na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema sifa hizo mpya zitahusisha pia wahitimu wanaomaliza stashahada ambao wanataka kujiunga na shahada ya kwanza.

Alisema maboresho hayo yaliyofanyika, hayatakuwa ya mwisho na kwamba kila mara serikali itakapoona kuna umuhimu wa kupandisha vigezo hivyo kutokana na matakwa ya nchi kwa wakati huo, suala hilo litafanyika.

Akizungumzia sababu iliyofanya serikali kuchukua hatua hiyo, Prof. Ndalichako alisema “huwezi kutengeneza nguo kwa pamba iliyooza ukategemea nguo imara.”

“Ili kutengeneza elimu bora lazima uangalie input yako (wanafunzi wanaoingia kwenye mfumo wa elimu) ndiyo maana tukaanza na hili.

“Sekondari nako tunaboresha na mazingira ili elimu inayotolewa iwe bora na hata ufaulu upande, lengo letu ni kuiboresha elimu na siku zote ili kuboresha elimu lazima uangalia wanafunzi wako.”

Hatua ya serikali imekuja pia wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa waajiri kuwa wahitimu wa elimu ya juu nchini hushindwa kufanya vizuri kwenye soko la ajira.

SWALI: Kwa upande wa sekondari ni marekebisho gani mmefanya?

JIBU: Kwenye udahili wa mwaka huu, alama za kufanya wanafunzi waingie kidato cha tano ni tofauti na ilivyokuwa.

Kwa mwaka huu mwanafunzi lazima apate credit (ufaulu wa kuanzia alama C na kuendelea) mbili kwa masomo ambayo anaenda kusomea.

Mwanzoni ilikuwa unaweza kwenda kusoma labda HGL (Historia, Jiografia na Kingereza) hata kama kote umepata alama D, cha msingi tu ilikuwa uwe na hizo credit hata kwenye masomo mengine kwa mfano Civics, Dini na kwingineko, sasa hivi tukasema hapana, wachaguliwe kwenye masomo waliyofaulu.

Lengo ni kufikia mwanafunzi asome masomo yote matatu akiwa na credit, sema tu kwa sababu kuna changamoto za wengi kushindwa hesabu, tukasema kwanza tuanze hivi wakati tukiendelea na maboresho mengine.

Mazingira yakiendelea kuruhusu sifa zitakuwa zinaendelea kupitiwa, kulingana na mahitaji kitaifa.

SWALI: Vipi kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kusoma shahada ya kwanza?

JIBU: Sifa za wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu zimeboreshwa kuanzia mwaka huu pia, mwanzo alama za chini kabisa ili ujiunge na chuo kikuu ilikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha sita kupata angalau E mbili.

Alama E kwa kidato cha sita ni alama ya mwisho kabisa ya ufaulu (kama ilivyo D kwa kidato cha nne) sasa kama mtu wa chuo kikuu anaenda na kiwango cha chini kabisa cha ufaulu, wa Diploma (stashahada) ataenda na nini?

Kwa hiyo tumeziboresha kiasi. Sasa tumesema ili uende chuo kikuu angalau upate point 4 ambazo ni D mbili ama akipata C moja na E moja.

Hii ni kwa sababu D ni pointi mbili na C ni pointi tatu, na kadhalika, kwa hiyo tukisema pointi nne, inamaana ukiwa na D mbili inakuwa ni pointi nne. Kwa maana hiyo akipata C ni pointi tatu na E ni moja.

Swali: Vipi kwa waliohitimu stashahada na sasa wanataka kuendelea kwa ngazi ya shahada?

Jibu: Na hao pia zimepandishwa, hao wa diploma (stashahada) wanahesabika kwa GPA ambao vigezo vya mwaka huu ni 3.5 ambayo imepanda kutoka 2.7.

Kwa wale wasiotumia GPA basi tumesema wapate wastani wa B+ ndio uweze kujiunga na chuo kikuu na sifa hizo pia zimeanza mwaka huu.

Swali: Kwa ujumla unadhani kuna changamoto kiasi gani kwenye elimu ya juu?

JIBU: Kwenye masomo ya vyuo vikuu bado kuna changamoto kwa sababu unaweza kukuta fani moja ya uhandisi inafundishwa na vyuo mbalimbali, vingine vya serikali vingine vya binafsi sasa TCU (Tume ya Vyuo vikuu) ambayo inaangalia ubora wa elimu na kinachoendelea chuoni ilikuwa haijaweka utaratibu kuangalia ulinganifu wa mhandisi anayetoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni sawa na anayetoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph? Hilo lilikuwa halijafanyika ndiyo maana kwenye soko la ajira unapata malalamiko ya uwezo wa wahitimu wetu.

Sasa tunaangalia vitu vingi, hilo la kuangalia wahitimu wetu tuone TCU ifanyeje kuboresha hayo, ingawa halijafanyika bado ila litafanyika.

Lazima tuangalie sheria ya vyuo vikuu, ubora wa vyuo kwa kuangalia vigezo vya kusajili vyuo, tumetambua kuna utapeli.
Baadhi ya vyuo vinaanzisha fani; kabla hajasajiliwa wanaanza kuchukua wanafunzi. Kwenye mapitio ya sheria tunataka wanaofanya hivi wabanwe.

Kuwabana pia wanaodahili wanafunzi wasio na sifa kwa sababu sasa wanafunzi ndiyo wanaumia kwa kuwa kama umesajiliwa bila sifa utaachishwa masomo.

Lakini pia tunaangalia mapitio ya Nacte (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi) kwa sababu kwa sasa Nacte wanasajili mpaka shahada ya uzamili, na TCU nao hivyohivyo, unakuta nusu ya vyuo vipo TCU na vingine Nacte, hiyo ni shida, wasiyo waaminifu vyuoni wanatumia huo mwanya kufanya utapeli.

Unakuta chuo kinaanzisha fani bila kuisajili, ukienda Nacte wanakwambia hicho ni Chuo Kikuu kipo chini ya TCU; ukienda TCU wanasema cheti kipo Nacte, kwa hiyo lazima tuangalie hilo.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mwisho wa ‘vilaza’ elimu ya juu rasmi. Mwisho wa ‘vilaza’ elimu ya juu rasmi. Reviewed by Zero Degree on 8/23/2016 10:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.