Loading...

Siri yafichuka Yanga

Katibu wa Yanga Baraka Deusdedit.

IMEBAIKIKA kuwa chanzo cha wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Yanga kufanya vibaya ni wachezaji wake kutolipwa mishahara.



Habari kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga inayoshiriki michuano ya kimataifa zinasema hawajalipwa mishahara ya miezi miwili na hivyo wachezaji wamevunjika moyo.

Yanga haijapata matokeo mazuri katika mechi zake nne za Kombe la Shirikisho Afrika ambapo imepoteza mechi tatu na kutoka sare mechi moja.

Timu hiyo kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya kucheza na Mo Bejaia ya Algeria katika mechi nyingine ya michuano hiyo itakayochezwa Agosti 13 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumzia hilo, Katibu wa Yanga Baraka Deusdedit alikanusha taarifa hizo akisema hakuna mchezaji ambaye hajalipwa.

Alisema hadi kufikia sasa hakuna mchezaji yeyote anayeidai timu hiyo na huo ni utaratibu ambao wamejiwekea siku nyingi wa kulipa mishahara mapema ili kuwaongezea ari ya kujituma na kupata matokeo mazuri kwenye za michuano hiyo.

“Kama wanadai basi labda ni mshahara wa mwezi ujao, lakini hadi sasa hakuna mchezaji ambaye hajalipwa mshahara wake na hizo ni taarifa ambazo zina mpango wa kutaka kutuvuruga, lakini sisi kama uongozi tupo makini na matokeo tunayoyapata tunaamini ni ya kimichezo na hayatokani na wachezaji wetu kucheza chini ya kiwango,”alisema Deusdedit.

Katibu huyo alisema zipo changamoto nyingi wanazokumbana nazo hivi sasa hadi kushindwa kufanya vizuri, mojawapo likiwa ni ugeni wao katika michuano hiyo, lakini wanafurahishwa na kiwango na jitihada zinazooneshwa na wachezaji wao hadi kufika hapo walipo.

Katika hatua nyingine, Deusdedit alisema pamoja na kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi hilo hawajakata tamaa na kikosi chao kipo kwenye maandalizi makali kujiandaa na mchezo wao ujao dhidi ya Mo Bejaia ambao utapigwa Agosti 13, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

“Pamoja na kwamba nafasi yetu ni ndogo kucheza nusu fainali, lakini tunataka kumaliza kwa heshima kuhakikisha tunashinda mechi zetu mbili zilizobaki tukianza na Mo Bejaia na ile ya mwisho dhidi ya TP Mazembe,”alisema.

Aidha kiongozi huyo alisema maandalizi hayo yamelenga pia kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lengo likiwa ni kutetea taji lao ambalo wanalishikilia kwa misimu miwili mfululizo.


Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Siri yafichuka Yanga Siri yafichuka Yanga Reviewed by Zero Degree on 8/02/2016 10:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.