Loading...

Profesa awasisitiza wachezaji kupima afya.

PROFESA Mohamed Janabi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
PROFESA Mohamed Janabi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ameshauri wachezaji kupimwa afya kabla ya kuanza kwa mashindano.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Profesa Janabi alisema kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linashauri kabla ya mashindano yoyote kuanza wachezaji wafanyiwe vipimo) ili kujua afya zao kwa sababu wengine wanazaliwa wakiwa na moyo mkubwa hivyo inasaidia kupunguza athari zinazoweza kutokea uwanjani.

Kauli hiyo ya Profesa Janabi imekuja baada ya kifo cha mchezaji wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Mbao, Ismail Khalfan aliyefikwa na umauti baada ya kugongana mwenzake wa Mwadui wakati timu hizo zikicheza mechi ya ligi ya vijana kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera.



Kwa mujibu wa jopo la madaktari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mchezaji huyo alipata shambulio la moyo ghafla ambapo moyo wake ulisimama na kumsababishia mauti.




“Wachezaji wafanyiwe vipimo kabla ya kuanza kwa mashindano pia kwenye viwanja pawepo na mashine maalumu ya kushtua moyo pale mchezaji atakapopata tatizo la moyo kusimama ghafla akiwa mchezoni,” alisema Profesa Janabi.

Pia Profesa Janabi alisema utafiti uliofanyika na FIFA katika nchi 170 ambazo ni mwanachama kila mwezi mchezaji mmoja anaanguka uwanjani, hivyo kufanya vipimo ni muhimu kwa wachezaji kwani haichukui saa moja kwa mchezaji mmoja.

Profesa Janabi alisema mashine ya kushtua moyo inabandikwa kifuani na inasoma kama moyo unafanya kazi na endapo moyo haufanyi kazi inapiga shoti moyo na kusaidia mapigo kushtuka na kuendelea kufanya kazi huku mchezaji akipatiwa matibabu.

“Mashine hii ni rahisi kubeba kwani haizidi kilo moja na ni rahisi kutumia,” alisema Profesa Janabi.

Profesa Janabi alisema wanamichezo wanatakiwa kufahamu kawaida moyo una mfumo wa umeme ambao unadhibiti mapigo ya moyo, mfumo huu ukisimama basi moyo unashindwa kusukuma damu sehemu muhimu kama ubongo na ogani kuu.

“Moyo ukisimama bila kurudi katika hali yake unasababisha kifo ndani ya sekunde chache na njia pekee ya msaada ni kupita ‘electrical shock’ ili kushtua mfumo wa umeme wa moyo, na hii inapaswa kufanyika ndani ya sekunde chache mno,” alisema.


ZeroDegree.
Profesa awasisitiza wachezaji kupima afya. Profesa awasisitiza wachezaji kupima afya. Reviewed by Zero Degree on 12/07/2016 10:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.