Loading...

Wazee wa Simba SC wauzuia mkutano ulioitishwa na uongozi wa klabu disemba 11.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Hamisi Kilomoni.
BARAZA la Wadhamini la Simba limezuia Mkutano Mkuu maalum wa wanachama uliotishwa na uongozi wa klabu Desemba 11, mwaka huu hadi kwanza ufanyike uhakiki wa wanachama wote.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Hamisi Kilomoni alisema kwamba wameuzuia mkutano huo kwa sababu ni matokeo ya mkutano batili uliofanyika Julai 31 mwaka huu. 

Kilomoni alisema kwamba wanachama wengi waliingia kwenye Mkutano wa Julai 31 kwa kuonyesha risiti badala ya kadi za uanachama, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba.

Ikumbukwe Mkutano huo ndiyo ulipitisha azimio la mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuuziwa asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. Bilioni 20.

Kilomoni jana alisema kwamba pamoja na uhakiki wa wanachama utakaosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu, pia klabu inapaswa kutoa elimu ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kwa wanachama wote Tanzania nzima kupitia matawi.

“Kwa kuwa sisi wadhamini hatujashirikishwa hata mara moja katika jambo kubwa kama hilo, ambalo linagusa mali za Simba, hivyo tunamuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndugu Paul Makonda kusimamisha Mkutano wa Desemba 11, kwani kuna kila dalili za uvunjifu wa amani kutokana na mgawanyiko wa wanachama na chuki zilizopandikizwa kama Mkutano wa mwanzo wa Julai 31, ambao Rais wa Simba, Evans Aveva alitolewa kwa ulinzi mkali wa Polisi,”alisema Kolomoni na kuongeza;

“Tunaiomba Serikali iingilie kati mgogoro huu kwa ajili ya usalama wa nchi,”. Mapema jana, Rais wa Simba, Aveva aliitisha mkutano na viongozi wote wa matawi Dar es Salaam Jumamosi makao makuu ya klabu kujadili mkutano wa Desemba 11.

Ajenda kuu ya Mkutano wa Desemba 11 ni mabadiliko ya Katiba ili kupata mpya itakayoruhusu mfumo mpya wa uendeshwaji kwa kuuza hisa.

Na mkutano huo uliitishwa baada ya agizo la Serikali kuzuia mchakato wa mabadiliko hadi kwanza marekebisho ya katiba yafanyike.

Lakini tayari Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limekwishakataza mpango wa kuzikabidhi klabu kongwe nchini, Simba na Yanga kwa mmiliki mmoja mmoja, bali zibaki kuwa za wanachama wengi kama zilivyo.

ZeroDegree.
Wazee wa Simba SC wauzuia mkutano ulioitishwa na uongozi wa klabu disemba 11. Wazee wa Simba SC wauzuia mkutano ulioitishwa na uongozi wa klabu disemba 11. Reviewed by Zero Degree on 12/03/2016 09:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.