Loading...

Yanga ruksa kutumia Uwanja wa Taifa.


HATIMAYE klabu ya Yanga imesaini mkataba rasmi na serikali kwa ajili ya kutumia Uwanja wa Taifa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopangwa kuanza rasmi Desemba 17 mwaka huu.

Serikali imesaini mkataba huo na Yanga utakaoiwezesha klabu hiyo ya Jangwani kutumia Uwanja wa Uhuru na ule wa Taifa katika mechi zake za Ligi na zile za kimataifa.

Mkataba huo umesainiwa jana, na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya Serikali na Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit.

Katika Mkataba huo, Klabu ya Yanga imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa sharti la kuvitunza wakati wote wanapovitumia.

Miongoni mwa masharti hayo ni kutunza viwanja, mali na vifaa vyote vilivyopo katika viwanja hivyo, na endapo kutatokea uharibifu wowote utakaofanywa na wachezaji ama mashabiki, Klabu hiyo itawajibika kubeba gharama za matengenezo yote yatakayotokana na uharibifu huo.

Aidha, Klabu ya Yanga inaweza kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi ya kujiandaa na mechi zinazowakabili.

Serikai ilifikia azma ya kuzifungia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa baada ya mechi yao ya Ligi iliyochezwa Oktoba mosi mwaka huu, kuzuka vurugu kubwa zilizofanywa na mashabiki wa Simba baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.

Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga na kuusogeza kwa mkono mpira kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.

Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Katika vurugu hizo, Saanya akamtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.

Wakati huo huo, Waziri wa Habar,i Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye leo atakagua Uwanja wa Taifa na kujionea ukarabati uliofanyika mara baada ya tukio la mashabiki wa soka kuharibu miundo mbinu iliyopo ndani ya uwanja huo.

ZeroDegree.
Yanga ruksa kutumia Uwanja wa Taifa. Yanga ruksa kutumia Uwanja wa Taifa. Reviewed by Zero Degree on 12/03/2016 12:39:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.