Loading...

Mechi ya Simba na Yanga yasogezwa mbele

MCHEZO wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya mahasimu, Simba na Yanga umesogezwa mbele kwa wiki moja na sasa utachezwa Februari 25 mwaka huu.

Awali mchezo huo ulikuwa umepangwa kuchezwa Februari 18. 

Habari kutoka ndani ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba sababu ya kusogezwa mbele kwa mchezo huo kunatokana na muingiliano na ratiba ya Shirikisho la soka Afrika (CAF)ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Februari 10, mwaka huu, Yanga watakuwa wageni wa Ngaya FC katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Mde mjini Mde nchini Comoro, kabla ya kurudiana Februari 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa sababu hiyo, bodi ya ligi imeona mchezo huo wa Simba na Yanga hauwezi kufanyika tena Februari 18 na imeamua kuusogeza mbele kwa wiki moja.

Wakati huo huo, Uongozi wa klabu ya Yanga jana umewasilisha barua kwa Wizara ya Habari Sanaa na Utamaduni na Michezo, kuomba iruhusiwe kuanzia mwisho wa wiki hii kuutumia Uwanja wa Taifa kwenye michezo yake ya ligi kuu badala ya uwanja wa Uhuru wanaoutumia sasa kufuatia Serikali kupitia Wizara hiyo kuzipiga marufuku Simba na Yanga kuutumia uwanja wa Taifa baada ya mashabiki wanaosadikiwa kuwa ni wa Simba kuvunja viti wakati wa mchezo wa mahasimu hao mwaka jana.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit aliiambia Nipashe jana mjini Dar es Salaam kwamba ombi hilo linatokana kukaribia kuanza kucheza michezo yao ya michuano ya Afrika.

Baraka alisema wangependa kuona wanaanza kuutumia uwanja huo ili wachezaji waanze kuuzoea kabla ya michezo yao ya Kimataifa haijaanza.

“Kama unavyojua kwa muda mrefu hatujautumia Uwanja wa wetu huu kipenzi wa Taifa baada ya kuzuiwa na Serikali kufuatia vurugu za kwenye mechi yetu na Simba baada ya mashabiki wa wenzetu kufanya fujo na kuvunja viti, lakini pia kama utakumbuka baadaye sisi (Yanga) tuliingia mkataba maalum na Serikali wa kuutumia Uwanja huu kwa mechi za mashindano ya Afrika na ule wa Uhuru kwa Ligi Kuu pekee.

Hivyo kwa kuwa tunakaribia kuanza mechi za Afrika, tunaiomba Serikali ituruhusu kuhamishia mechi zetu za mashindano ya nyumbani Uwanja wa Taifa, ili iwe sehemu ya maandalizi yetu ya michuano hiyo ya Afrika,”alisema Baraka.

Yanga watakuwa wenyeji wa Mwadui ya Shinyanga Januari 29 mjini Dar es Salaam na baada ya hapo, itaikaribisha Stand United Februari 5, mwaka huu kabla ya kuingia kwenye michuano ya Afrika.

ZeroDegree.
Mechi ya Simba na Yanga yasogezwa mbele Mechi ya Simba na Yanga yasogezwa mbele Reviewed by Zero Degree on 1/24/2017 11:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.