Loading...

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kuapishwa leo Ijumaa Tarehe 20 January, 2017

Trump aliweka picha hii kwenye ukurasa wake wa Twitter na kusema alikuwa anaandika hotuba atakayoisoma baada ya kuapishwa
RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump anaapishwa leo kuongoza nchi hiyo. Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo viongozi wake wanaochaguliwa, huwachukua wiki kadhaa kabla ya kukabidhiwa madaraka.

Baada ya uchaguzi, kura zikishaamua, mshindi huunda baraza la mawaziri na kuanza kuunda sera kamilifu ya uongozi.

Wakati huo huo, rais anayeondoka inaelezwa kwamba, hujitahidi kuacha sifa nzuri ya uongozi wake kabla ya kuondoka Ikulu. Kwa mujibu wa katiba ya Marekani, rais anaapishwa Januari 20 ya mwaka unaofuata uchaguzi ulipofanyika.

Marekani ambayo hupitisha zaidi ya wiki 11 kabla ya rais kuapishwa, hufanya hivyo kwa ajili ya kumpa rais ajaye muda wa kuteua baraza lake la mawaziri na kuweka mipango kwa uongozi mpya. Januari 20 ni siku ambayo Marekani imeiteua kikatiba kuwa maalumu kwa ajili ya kuapisha marais.

Historia inaonesha, tangu mwaka 1936, marais wa nchi wamekuwa wakiapishwa tarehe hii ya leo. Ikitokea tarehe hii ikaangukia Jumapili, basi huapishwa kimya kimya na kisha sherehe hufanyika kesho yake; kwa maana ya Jumatatu. Asili ya kuapishwa rais na makamu wake ilikuwa Machi 4 .

Tofauti na George Washington aliyeapishwa Aprili 30, 1789, viongozi wengine walikabidhiwa ofisi Machi 4 au Machi 5 endapo ilitokea hiyo siku ikaangukia Jumapili. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya 20 ya katiba ya Marekani yaliyopitishwa Januari 23, 1933, yalibadilisha tarehe ya kuapishwa kutoka Machi 4 na kuwa Januari 20. Mabadiliko hayo ya 20 ya katiba yaliyobatizwa ‘The Lame Duck Amendment’.

Mabadiliko hayo yalifupisha muda wa wanasiasa hao; rais na wajumbe wa Congress kubaki kwenye ofisi baada ya uchaguzi. Kwa hiyo, uapisho wa rais ukafanywa uwe Januari 20 huku upande wa wajumbe wa baraza la Congress ikipangwa Januari 4.

Rais Franklin Roosevelt ndiye alikuwa wa kwanza kuapishwa Januari 20, mwaka 1937 aliposhika awamu ya pili ya uongozi.

Kwa kuwa siku hiyo iliangukia Jumapili, aliapishwa peke yake na sherehe zilifanyika kesho yake. Hitimisho la Obama Barack Obama aliyeapishwa tarehe kama ya leo, 2009 kuwa rais wa 44, hivi karibuni alitoa hotuba ya kuwaaga Wamarekani tayari kwa kumpisha Trump leo.

Katika hotuba yake ya mwisho aliyoitoa mjini Chicago, amehimiza Wamarekani kuitetea demokrasia. Obama ndiye rais wa kwanza Marekani mwenye asili ya Afrika aliyechaguliwa mwaka 2008.

Trump ambaye sasa anakuwa rais wa 45 kuongoza taifa hilo kubwa, ameahidi kubatilisha baadhi ya sera kuu alizofanikisha Obama.

Rais wa Marekani huchaguliwa kupitia mfumo wa kura za wajumbe, ambapo rais huchaguliwa kwa muhula wa miaka minne.

Inawezekana pia kwamba rais achaguliwe kupitia katika Bunge Dogo la Wajumbe (US House of Representatives), ikiwa kongamano la wajumbe halikuweza kumchagua rais kwa kumpa mgombea mmoja kura nyingi kuliko mwingine yeyote.

Kulingana na Katiba ya Marekani, mtu yeyote hawezi kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo zaidi ya mara mbili. Kukitokea kifo, kujiuzulu au kuondolewa madarakani kwa rais, Makamu wa Rais wa Marekani atachukulia kiti cha rais. Idadi ya marais walioapishwa kutokana na Katiba ya Marekani ya Machi 4, 1789 ni 43 (Trump anakuwa wa 44). Kumekuwa na marais 44 walioongoza nchi hiyo (baada ya Trump kuapishwa leo idadi inakuwa 45). Rais Grover Cleveland alitumikia mihula miwili isiyofuatana hivyo huhesabiwa mara mbili, kama rais wa 22 na wa 24. Aidha, marais wanne walifariki wakiwa madarakani.

Nao ni William Henry Harrison, Zachary Taylor, Warren G. Harding, na Franklin D. Roosevelt. Mwingine, Richard Nixon alijiuzulu na wanne wakauawa.

Waliouawa ni Abraham Lincoln, James A. Garfield, William McKinley, na John F. Kennedy. Rais wa kwanza wa Marekani alikuwa George Washington, aliyeapishwa 1789 baada ya kupigiwa kura na wajumbe wote katika kongamano.

William Henry Harrison alitumikia kwa siku 31 pekee, mwaka 1841, naye Franklin D. Roosevelt akahudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko wote; miaka 12. Marais wote

Ifuatayo ni orodha ya marais wa Marekani na vipindi vyao vya utawala katika mabano: George Washington (1789 - 1797), John Adams ( 1797 – 1801), Thomas Jefferson (1801 – 1809), James Madison (1809 – 1817), James Monroe (1817 – 1825), John Quincy Adams (1825 – 1829), Andrew Jackson (1829 – 1837).

Martin Van Buren (1837 – 1841), William Harrison (1841), John Tyler (1841 – 1845), James Polk (1845 – 1849), Zachary Taylor (1849 – 1850), Millard Fillmore (1850 – 1853), Franklin Pierce (1853 – 1857), James Buchanan (1857 – 1861), Abraham Lincoln (1861 – 1865).

Wengine ni Andrew Johnson (1865 – 1869), Ulysses Grant (1869 – 1877), Rutherford Hayes ( 1877 – 1881), James Garfield (1881 – 1881), Chester Arthur (1881 – 1885), Grover Cleveland (1885 – 1889), Benjamin Harrison (1889 – 1893), Grover Cleveland (1893 – 1897), William McKinley (1897 – 1901).

Marais wengine walioiongoza Marekani ni Theodore Roosevelt (1901 – 1909), William Howard Taft (1909 – 1913), Woodrow Wilson (1913 – 1921), Warren Harding (1921 – 1923), Calvin Coolidge (1923 – 1929), Herbert Hoover (1929 – 1933), Franklin Roosevelt (1933 – 1945), Harry Truman (1945 – 1953) na Dwight Eisenhower (1953 – 1961).

Wengine ni John Kennedy (1961 – 1963), Lyndon Johnson (1963 – 1969), Richard Nixon (1969 – 1974), Gerald Ford (1974 – 1977), Jimmy Carter (1977 – 1981), Ronald Reagan (1981 – 1989), George H. W. Bush (1989 – 1993), Bill Clinton (1993 – 2001), George W. Bush (2001 – 2009), Barack Obama (2009 – 2017) .

Sasa Januari 20 iliyoidhinishwa kikatiba kuwa siku ya uapisho wa rais, leo inaandika historia mpya kwa kuipatia Marekani rais wa 45 ambaye ni Donald Trump.

Hivyo Wamarekani leo wanampa mkono wa kwaheri Obama na kumkaribisha Trump Ikulu.

Makala haya yameandaliwa na Stella Nyemenohi kwa msaada wa vyanzo mbalimbali katika mtandao wa intaneti.

ZeroDegree.
Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kuapishwa leo Ijumaa Tarehe 20 January, 2017 Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kuapishwa leo Ijumaa Tarehe 20 January, 2017 Reviewed by Zero Degree on 1/20/2017 09:56:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.