Loading...

Rais Museveni amkaribisha Bakhresa nchini Uganda

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda ameikaribisha Kampuni ya Bakhresa Group na wawekezaji wengine wa Kitanzania kuwekeza katika nchi yake. Akizungumza baada ya kutembelea viwanda vya kusaga nafaka na juisi vinavyomilikiwa na Kampuni ya Bakhresa Group eneo la Tazara na Vingunguti Dar es Salaam jana, Rais Museveni alisema kwa kufanya hivyo kutaifanya nchi hiyo kupata fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani.

“Sikuijua kampuni hii, lakini naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kunileta hapa. Tangu mwanzoni chama chetu cha siasa kinaamini katika utengamano wa wima (vertical integration), hususani kusindika mazao na uzalishaji mwingine ambapo mazao kutoka shambani husindikwa mpaka yanapokwenda kwa ajili ya matumizi au sokoni kuuzwa,” alieleza Rais Museveni aliyekuwa na ziara ya siku mbili nchini.

Alisema uwekezaji kama huo utasaidia kuzalisha bidhaa za ndani na kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuitolea mfano Bakhresa Group kuwa ni nzuri kwa sababu ni kiunganishi katika hatua mbalimbali za uzalishaji, na inaokoa fedha kwa Tanzania, Uganda na kuokoa fedha za kigeni, lakini pia inapata fedha za kigeni kwa kuuza nje bidhaa zao. Rais Museveni aliongeza:

“Uganda inapeleka India dola za Marekani bilioni 1.5 kila mwaka, tunauza nje mahindi mengi ambayo hayajasindikwa, yakiwa ghafi, jambo linalotufanya tupate fedha kidogo, hivyo nawakaribisha (Bakhressa) Uganda kwa ajili ya kusindika mahindi.”

Awali, akimpa maelezo Rais Museveni, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni za Bakhresa Group, Hussein Sufian alisema ndani ya miaka miwili ijayo, kampuni hiyo inaongeza uwekezaji kwa kujenga kiwanda kipya cha kusaga mahindi nchini Uganda.

Alisema kiwanda hicho ambacho kitakuwa na uwezo wa kusaga wastani wa tani 500 za mahindi kwa siku, kinakwenda sanjari na ujenzi wa ghala za kuhifadhia bidhaa hizo ambao uwekezaji wake una thamani ya dola za Marekani milioni 50.

Sufian alisema kwa sasa Bakhresa Group imewekeza kwa kujenga kiwanda cha kusaga chenye uwezo wa kusaga wastani wa tani 1,100 kwa siku na uwekezaji huo ulifanyika tangu mwaka 1998 ambapo mpaka sasa jumla ya dola za Marekani milioni 60 zimewekezwa katika kiwanda hicho.

“Kampuni ina mipango ya kuongeza uwekezaji wake nchini Uganda na kwa sasa tuna mipango ya kuongeza ukubwa wa kiwanda kilichopo ili kiongeze uzalishaji wa ngano kutoka tani 1,100 kwa siku hadi kufikia tani 2,000 kwa siku,” alisema na kuongeza kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira ya watu 650 nchini Uganda.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania na Waganda kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika viwanda nchini.

“Bakhresa ameanza na anatumia wastani wa tani 30,000 za matunda kwa mwaka wakati uwezo wa Tanzania kuzalisha matunda ni tani milioni nne,” alisema Mwijage na kupongeza kuwa mbali na kiwanda hicho, pia viwanda vitatu vya kusindika matunda vitajengwa nchini katika eneo la Kijiji cha Mboga mkoani Pwani, Mbeya na Mwanza ili kutumia uzalishaji wa matunda tani milioni nne zinazozalishwa.
Rais Museveni amkaribisha Bakhresa nchini Uganda Rais Museveni amkaribisha Bakhresa nchini Uganda Reviewed by Zero Degree on 2/27/2017 12:02:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.