Jinsi Kocha Lwandamina alivyoigawa Yanga
Kocha George Lwandamina |
Wanachama na mashabiki wa Yanga jijini Mwanza wamemtaka kocha George Lwandamina kuondoka na mabegi yake wakati timu hiyo itapokwenda Zambia kurudiana na Zanaco wiki ijayo.
Yanga itacheza mechi yake ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ugenini Jumamosi ijayo ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare 1-1 na Wazambia hao Jumamosi iliyopita.
Wanachama hao, Emmanuel Majura “Emma Yanga” na Mzamiru Abeid walisema kuwa kutokana na matokeo mabovu wanayoyapata wao wanachama ndio wanaoumia zaidi na kusisitiza kocha huyo aondoke.
Walisema akiondoka ni bora aende na mabegi yake na asirudi kwani hawajaona kipya walichokifanya tangu akabidhiwe timu hiyo.
Majura alisema kuwa kocha huyo ameanza kuwapotezea hata matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kutokana na kushindwa kupanga vizuri hata kikosi.
“Kocha huyu (Lwandamina) bora aondoke tena haraka hajatufanyia lolote tangu afike hapa, tumeshuhudia timu inacheza chini ya kiwango na kusababisha sisi wanachama kuumia tu,” alisema Majura.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Abeid ambaye alisema Lwandamina hajaleta mabadiliko yoyote kama walivyotarajia na kushauri arejeshwe kikosini Hans Pluijm.
“Naunga mkono kuondoka kwa Lwandamina, tena bahati nzuri Yanga inaelekea huko kwao (Zambia) bora akusanye mabegi yake aondoke nayo,” alisema Abeid.
Katibu wa Yanga tawi la Mwanza, Khamis Maluli na alisema kuwa kocha huyo apewe muda hadi ligi iishe.
Alisema kuwa suala la matokeo kuwa mabovu ni hali ya mpira na kwamba bado ni mapema kwa Mzambia huyo kulaumiwa.
“Apewe muda tu, aangaliwe kama Arsenal kocha wao (Arsene Wenger), amedumu kwa muda gani na matokeo gani amepata sasa hivi? Tumpe muda Lwandamina,” alisema Maluli.
Source: Mwananchi
Jinsi Kocha Lwandamina alivyoigawa Yanga
Reviewed by Zero Degree
on
3/14/2017 01:13:00 PM
Rating: