Loading...

Kocha Omog na siri nzito Kanda ya Ziwa

LICHA ya Simba kuwa na kibarua kigumu kuelekea kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa msimu huu pale itakapocheza michezo mitatu Kanda ya Ziwa, kocha wa timu hiyo, Mcameroon Joseph Omog ana siri nzito ya kupata matokeo.

Ikumbukwe kuwa mechi hizo ndizo zitakazotoa picha kamili ya ubingwa msimu huu.

Simba itaanza kucheza na Kagera Sugar Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na siku sita baadaye itashuka katika Uwanja wa CCM Kirumba kucheza na Mbao FC na baada ya siku nne itacheza na Toto African kwenye dimba hilo.

Kocha wa Simba, Joseph Omog kwa kutambua umuhimu wa michezo hiyo ya ugenini, ameandaa mkakati maalum kuhakikisha wanavuna pointi zote tisa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog alisema kuwa anafahamu ugumu wa michezo hiyo ya ugenini na anachokifanya kwa sasa ni kuandaa timu yake kukabiliana na ushindani wowote kutoka kwa wapinzani wao hao.

"Huwezi kusema kuwa hii ni michezo rahisi..., ni michezo migumu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu, tunachokifanya kwa sasa ni kuelekeza mawazo yetu kwenye michezo hii pamoja na kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha tunavuna pointi zote," alisema Omog.

Aidha, alisema kuwa, wanaendelea na maandalizi pamoja na kuwakosa baadhi ya nyota wake ambao wameteuliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars'.

"Kabla ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Madini, tayari kulikuwa na programu niliyokuwa nimeiandaa kuelekea kwenye michezo hii, niwatoe hofu mashabiki kwa kuwaambia timu ina ari ya ushindi," alisema Omog.

Kikosi cha Simba kilitegemewa kurejea Dar es Salaam jana kikitokea Arusha kilipokwenda kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Madini FC na kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililowapeleka hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Simba kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza michezo 24 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 53 wakiwa wamecheza idadi sawa ya mechi na vinara hao.

Source: Nipashe
Kocha Omog na siri nzito Kanda ya Ziwa Kocha Omog na siri nzito Kanda ya Ziwa Reviewed by Zero Degree on 3/22/2017 11:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.