Loading...

Magufuli amkaanga Mbunge wa Chama Cha Wananchi [CUF] kwa maswali haya mazito

RAIS John Magufuli alimbana kwa maswali mazito Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale Mwiru (CUF) katika tukio nadra kutokea majibizano ya maswali na majibu kati yao mbele ya wananchi waliokuwa wamekusanyika eneo la Somanga wilayani Kilwa mkoani Lindi, jana.

Ngombale ambaye alishinda ubunge dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa kikiongoza jimbo hilo, alikumbana na kibano cha maswali magumu wakati Rais Magufuli alipofika kwenye kata hiyo (Somanga) ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya siku nne kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Awali, mwananchi mmoja alimueleza Rais Magufuli juu ya mlolongo wa kero zinazowakabili ikiwamo ya ukosefu wa zahanati.

Mwananchi huyo alisema wanakabiliwa na hali ngumu ya kupata huduma za afya na kwamba, ikitokea mtu anaugua ghafla, hulazimika kukodi gari kwenda katika kituo cha afya kilichopo mbali na kata hiyo.

Baada ya kusilikiza kero, ndipo Magufuli alipotoa fursa kwa Ngombale kueleza mipango yake kwa kuwa wananchi walimchagua na aliwaahidi kushughulikia matatizo yao ikiwamo hiyo ya ukosefu wa zahanati.

"Sasa nampa yeye (mbunge)… aanze kujinadi anafanyaje ili na mimi niweze kujinadi hapa," alisema Rais Magufuli.

"Mnajua ni kwa nini nazungumza hivi? ... kila mmoja aliyekuja kuomba kura alisema atafanya hivi, atafanya hivi.. si ndiyo? Na bahati nzuri wabunge wana hela, wanalipwa fedha za jimbo," alisema Magufuli. Sehemu ya mahojiano ya Magufuli na Mbunge Ngombale ilikuwa hivi:

DK. MAGUFULI: Hivi mpaka sasa umeshalipwa milioni ngapi za maendeleo ya Mfuko wa Jimbo?

MBUNGE: Safari hii (2016/2017) nimepatiwa Sh. milioni 34.8.

MAGUFULI: Tangu uingie bungeni zimeshafika ngapi?

MBUNGE: Hii ni mara ya pili.

MAGUFULI: Kwa hiyo zimefika Sh. ngapi?

MBUNGE: Kama milioni 70.

MAGUFULI: Umeshapewa milioni 70, hapa Somanga umewachia ngapi?

MBUNGE: Hapa Somaga nimewaachia Sh. milioni tatu, mara ya pili milioni moja na kuna shule ya msingi ya Marindego na nyingine katika kata nyingine.

DK. MAGUFULI: Sasa kwa nini usilete angalau kama Sh. milioni 10 ama 20 kwa ajili ya hospitali?

MBUNGE: Mheshimiwa Rais... (alikatishwa)

MAGUFULI: Niahidi … unazipeleka wapi fedha zote milioni 70, zote halafu unaleta Sh. milioni 3 tu. Ungeletea Sh. milioni 15 ili kusudi na mimi nichangie hapa tumalizane hapa hapa leo.

MBUNGE: Naahidi kwenye bajeti ya mwaka ujao.

MAGUFULI: Aaa… mimi nasema kwenye hizo Sh. milioni 70 kwa nini usilete? Si bado zipo, lete milioni 15 na mimi nichangie.

Jamani na mimi si mnataka nichangie na mbunge naye achangie au atueleze anapeleka wapi hizo fedha, mbunge analeta shida hapa wakati hospitali ndiYo inaleta shida aseme anachangia shilingi ngapi kabla sijaondoka hapa tena.

MBUNGE: Fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo zimekuja mara mbili.

MAGUFULI: Mheshimiwa mbunge unazungumza maneno mengi, umeshasema ulipatiwa milioni 70, sema utatoa Sh. milioni 15?

MBUNGE: Siyo kwa bajeti ya mwaka huu kwa kuwa tayari nimeshazigawa, fedha nyingine nimezipeleka kwenye kata nyingine. Nikisema nazileta hapa, nitakuwa nadanganya… msema kweli mpenzi wa Mungu.

MAGUFULI: Mbunge amekataa kuchangia hata Sh. 100,000, basi mimi nitachangia Sh. milioni 20, najua wananchi mmeelewa, hebu, Mkurugenzi njoo.

Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa, Zabron Bugingo, alisema halmashauri itatoa Sh. milioni 10 huku akiagizwa na Rais Magufuli itangazwe tenda mara moja kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.

"Lakini mheshimiwa mbunge umeniangusha, hivi ukiambiwa uende tena pale… (eneo la kata hiyo).

Ngoja nikuache labda utaleta kwa wakati wako, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi waisimamie hiyo hospitali ijengwe, siku nikija kufanya ziara ya hapa Somanga, kama itakuwa imekamilika, nije kuifungua.Tunataka mambo hapo hapo badala ya kuchengachenga…" alisema Magufuli.

MBUNGE AFUKUNGUKA

Baada ya kibano hicho kilichoonekana kuwa ni sawa na kumkaanga mbele ya wapiga kura wake, mbunge huyo alizungumza nan Nipashe na kudai kuwa kilichotokea ni "propaganda za kisiasa".

"Rais aliwavuta wananchi kuona kama wabunge wanapewa fedha nyingi ambazo pengine matumizi yake hayaeleweki," alisema.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mitaa (LAAC), aliongeza: "Yeye alikuwa anataka mimi nichangie katika fedha nilizozitoa… jambo hilo nilikuwa silitaki kwa sababu ningekubali kuchangia Sh. milioni 10 isingekuwa rahisi.

Kwake ni rahisi, kesho angeweza kuleta fedha, angemlazimisha Mkurugenzi kutoa Sh. milioni 10 aliyoiahidi, atanijia mimi mbunge nitoe hela niliyoiahidi. Je, nitaipata wapi hiyo hela?"

Alisema tayari alikuwa na mkakati wake ambao alishaongea na serikali ya kijiji kutoa eneo kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa kupatikana kwa kituo cha afya pamoja na shule ya sekondari na kwamba suala hilo tayari limeshafanyika na limeingizwa katika vikao vyao vya halmashauri.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ya mwaka 2009, Ibara ya 7(i), matumzi ya fedha za mfuko huo ni lazima yaidhinishwe na kamati ya mfuko huo katika kila jimbo husika, mbunge akiwa mwenyekiti na kwa kawaida huwa zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Source: Nipashe
Magufuli amkaanga Mbunge wa Chama Cha Wananchi [CUF] kwa maswali haya mazito Magufuli amkaanga Mbunge wa Chama Cha Wananchi [CUF] kwa maswali haya mazito Reviewed by Zero Degree on 3/03/2017 03:17:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.