Loading...

Vita ya Simba na Yanga yaanza upya

BAADA ya Yanga kuwa bize na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba michuano ya Kombe la FA, sasa vita ya ubingwa imerejea upya kila moja ikijipanga kushinda michezo yao yote iliyobakia ili kutwaa ubingwa.

Yanga walikuwa wameelekeza akili zao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia, ambapo walitolewa na sasa wamerejea kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, April mosi mwaka huu.

Katika michuano hiyo, Yanga walijikuta wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, huku wakitoka suluhu ya 0-0 ugenini na kutupwa kwenye Kombe la Shirikisho ambapo wamepangiwa kukutana na CM Alger ya nchini Algeria.

Kwa sasa Wanajangwani hao wameelekeza akili zao katika mchezo dhidi ya Azam FC, ambapo wanaamini kuwa wakishinda watakuwa wamejitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa kwa madai kuwa huo ndio mchezo mgumu kwao kati ya sita iliyobaki.

Wakati Yanga wao wakielekeza akili kwa Azam FC, kwa upande wao Simba baada ya kutinga hatua ya nusu fainali FA walipowafunga Madini FC ya Arusha, sasa wanajipanga kwenda kujizolea pointi tisa Kanda ya Ziwa.

Katika msimamo wa ligi, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 55, Yanga wakifuatia nafasi ya pili wakiwa na pointi 53 na timu yoyote itakayoteleza katika michezo iliyobakia inaweza kumwachia mwenzake nafasi ya kutwaa ubingwa.
Vita ya Simba na Yanga yaanza upya Vita ya Simba na Yanga yaanza upya Reviewed by Zero Degree on 3/22/2017 11:26:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.