Loading...

Wanasiasa wajadili hatima ya Nape kisiasa

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akifurahia jambo na mtangulizi wake, Nape Nnauye walipokutana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana wakati wa mchezo wa soka kati ya Taifa Stars na Botswana. Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi. Picha na Mtandao
Wanasiasa, wakiwamo wa vyama vya upinzani wamezungumzia hatima ya kisiasa ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye huku wakimshauri kurejea jimboni kwake kujiimarisha na kutokata tamaa.

Ushauri huo umekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kumwondoa katika nafasi hiyo.

Alhamisi iliyopita, Rais Magufuli alimteua Dk Harrison Mwakyembe kuchukua nafasi ya Nape na kumteua Profesa Palagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria kujaza nafasi ya Dk Mwakyembe.

Dalili za Nape kuingia katika msukosuko wa kiutawala zilianza Februari baada ya kujitokeza hadharani na kutoa angalizo kuhusu baadhi ya wasanii ambao walikuwa wametajwa kuhusika na matumizi au biashara ya dawa za kulevya.

Akiwa waziri anayewasimamia, alitaka busara itumike katika mapambano hayo akibainisha kwamba kinyume chake itakuwa ni kuchafua majina na umaarufu wa wasanii hao uliojengwa kwa muda mrefu ikiwa itabainika kuwa hawahusiki.

Pia ilionekana kama amepishana na mamlaka za juu jinsi alivyoshughulikia suala la kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group.

Aliondolewa madarakani Alhamisi iliyopita siku moja baada ya kupokea ripoti ya uvamizi wa studio za kampuni ya Clouds Media Group uliofanyika Machi 17.

Wanasiasa wazungumzia
Pamoja na misukosuko hiyo, baadhi ya wanasiasa wamemshauri asikate tamaa, badala yake asonge mbele akianza na kujiimarisha katika ubunge. Nape ni Mbunge wa Mtama, jimbo lililopo katika Mkoa wa Lindi.

Mbali ya ushauri huo, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alimtaka mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kutafuta sehemu salama kama amekorofishana na Serikali na chama chake.

“Kimsingi kama Nape ameshindana na wenzake kwenye CCM na serikalini, afanye uamuzi wa kuachana nao,” alisema Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara).

Alipoulizwa kama wako tayari kumpokea Chadema kama atahamia, Mnyika alisema: ‘Hilo nitalitolea maelezo kama atakuja.”

Kiongozi wa CUF, Abdul Kambaya alisema anaamini kwamba kutokana na misimamo aliyonayo Nape, hawezi kuyumbishwa na kilichomtokea.

“Ninamfahamu Nape kwa muda mrefu, sijawahi kumuona akiwa na msimamo dhaifu. Alishashindana na vijana wenzake pale CCM kwenye mikataba ya ufisadi mpaka wakataka kumfukuza uanachama, lakini Rais mstaafu Jakaya Kikwete akamchukua na kumpa ukuu wa wilaya kabla ya kumpa nafasi kwenye sekretarieti ya chama hicho,” alisema Kambaya.

Aliishauri Serikali kujenga nidhamu ya viongozi na watumishi wa Serikali ili kustawisha uongozi (utawala) wa sheria bila kujenga kiburi kwa wateule wa Rais.

Mwingine aliyezungumzia hatima ya Nape kisiasa ni Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku Msukuma ambaye alimtaka arudi jimboni Mtama kuwatumikia wananchi kwa kuwa ndiyo kazi aliyoiomba.

“Nape amebaki na ubunge ambao ndiyo aliuomba, uwaziri hakuuomba, alipewa na Rais ambaye akiona hakufanya vizuri anamtoa. Mimi namshauri tu arudi jimboni akawatumikie wananchi wake, kama mimi sasa hivi napiga mikutano huku jimboni,” alisema Msukuma alipopigwa simu kutoa maoni yake.

“Kwani huo uwaziri una nini? Wanatuzidi Sh200,000 tu, hata kama ni gari si tulipewa mkopo wa Sh90 milioni? Kama alizila atafute nyingine. Arudi tu jimboni, kwanza wapiga kura wake wamem-miss,” alisema Msukuma.

Mpinzani mkubwa wa Nape katika Jimbo la Mtama, Suleiman Mathew alisema waziri huyo wa zamani amevuna alichopanda.

Mwenyekiti huyo wa Chadema Mkoa wa Lindi ambaye aligombea ubunge wa Mtama akichuana na Nape alisema japo anamsikitikia, Nape atabaki kuwa mpinzani wake.

“Mimi ni mwenyekiti wa chama wa mkoa, kazi yangu ni kuhakikisha kuwa tunapata majimbo yote.

Alipotafutwa ili azungumzie mustakabali wake kisiasa, Nape alitaka aachwe kwanza.

“Hata kama ni masuala ya wanahabari, aulizwe Waziri Mwakyembe, yeye anaweza kuzungumza, mimi niachwe kwanza,” alisema.

Source: Mwananchi
Wanasiasa wajadili hatima ya Nape kisiasa Wanasiasa wajadili hatima ya Nape kisiasa Reviewed by Zero Degree on 3/26/2017 04:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.