Loading...

Hii ndio sababu ya wabunge kumshangilia JK

Miaka sita iliyopita, Bunge liligawanyika wakati rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alipoingia bungeni kutoa hotuba ya kulizindua; wapinzani walisimama na kutoka nje, CCM wakabaki wakiwazomea.

Jana ilikuwa tofauti; wabunge wa vyama vyote walipiga kelele kushangilia mara alipotangazwa kuwa angeingia ukumbi wa Bunge na kelele zikawa maradufu alipotambulishwa, na wote walikuwa na sababu za shangwe hizo.

“Kushangilia kulikuwa na lengo la kuionyesha jamii kuwa kiwango cha uongozi cha Kikwete kilikuwa ni juu.,” alisema mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa baada ya kutoka ukumbini.

Kikwete, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Nne, alitinga bungeni kumsindikiza mkewe, Salma ambaye jana alikuwa anaapishwa baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.

Tofauti na miaka ya nyuma wakati alipokuwa akiingia kwenye ukumbi huo akiwa mbunge, waziri na baadaye Rais, Kikwete jana alikaa sehemu ya wageni, na hata juhudi za kutaka Bunge livunje kanuni ili aingie sehemu wanayokaa watunga sheria, hazikufanikiwa.

Kikwete, aliyeongozana na mtoto wake anayeitwa Ally, aliwasili ndani ya ukumbi wa Bunge saa 2:55 asubuhi.

Tofauti na siku nyingine ambazo Spika Job Ndugai hutambulisha wageni baada ya kipindi cha maswali na majibu, jana alibadili utaratibu kwa kumtambulisha Rais Kikwete kabla ya kipindi cha maswali na majibu mara baada ya Mama Salma kuapishwa.

“Nilikuwa nasubiri kidogo nione Mama (Salma Kikwete) anakaa wapi. Naomba nichukue fursa hii kuwatambulisha wageni maalumu walio katika gallery ya Spika,” alisema Spika Ndugai mara baada ya kuapishwa kwa Mama Salma.

“Na mgeni wetu wa siku ya leo, si mwingine bali ni Rais mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete.”

Kabla hajamaliza wabunge wote walianza kupiga makofi, vigelegele na kelele za shangwe zilizodumu kwa takriban dakika tatu.

Akiwa eneo hilo la wageni, Rais Kikwete alisimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kushukuru, lakini kelele hizo ziliendelea na kumlazimisha kiongozi huyo kunyoosha mikono tena kuwashukuru.

“Kwa makofi hayo, sasa naomba mumpe standing ovation (kumuonyesha heshima kwa kusimama,” alisema Spika Ndugai.

Ndipo wabunge waliposimama na kuendelea kupiga meza kwa nguvu kushangilia, huku Kikwete akinyoosha tena mkono kuwashukuru.

“Tunakumiss, tunakumiss,” zilisikika sauti za baadhi wa wabunge waliofungua vipaza sauti vyao kunogesha shangwe hizo.

Baadaye, Spika Ndugai alieleza yake ya moyoni.

“Waheshimiwa wabunge, binafsi mimi ni kipindi cha nne (bungeni), sijawahi kuona mgeni amepokewa kwa kiwango hiki,” alisema Spika.

Aliposema hayo, wabunge walilipuka tena kwa shangwe.

Licha ya kuwasihi wabunge hao na kuwataka watulie, waliendelea kushangilia huku baadhi wakitaka watengue kanuni ili Rais Kikwete aingie ndani ya Bunge na kusalimiana na Spika.

“Kwa kushangilia huko inaonyesha kuwa hata waliommiss wapo,” alisema Ndugai.

Alipoulizwa nje ya ukumbi kuhusu mwongozo aliotaka kuomba, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema alitaka Spika amruhusu Kikwete aingie ndani ya ukumbi wa Bunge.

Hata hivyo, Ndugai hakulikubali jambo hilo na badala yake Bunge liliendelea na ratiba yake ya maswali na majibu.

Kikwete, aliyekaa ndani ya ukumbi wa Bunge kwa takribani dakika 30, aliondoka baada ya utambulisho huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti bungeni jana, wabunge wa upinzani walisema walimshangilia Rais Kikwete kwa sababu aliruhusu kukosolewa, kushauriwa na alikubali kuchukua ushauri wa watu tofauti.

“Tulimshangilia kwa sababu aliruhusu demokrasia,” alisema Mchungaji Msigwa.

“Kikwete alivumilia vitendo vya kutoka bungeni kwa sababu alifahamu kuwa hiyo ni demokrasia ambayo inafanyika kote duniani kama njia ya kuonyesha watu hawakubaliani na jambo fulani. Lakini hivi sasa tukifanya hivyo ananuna (bila kumtaja jina), alisema”

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema wakati walipokuwa wakimsusia Kikwete bungeni si kwamba walikuwa wanayakataa mambo yake yote.

“Kikwete aliruhusu kusema, kushauri na kukosolewa. Sasa watu wanasema Serikali inachukua hatua dhidi ya mafisadi, lakini kuna hatari ya kumuadhibu mtu kutokana na chuki binafsi tofauti na utawala uliopita,” alisema.

Kwa upande wake Zitto alisema wabunge wanamkumbuka mbunge huyo wa zamani wa Chalinze kwa kuwapa uhuru wa kusema chochote.

“Aliruhusu hata Bunge kubadilisha bajeti pale linapoona inafaa tofauti na sasa. Hivi sasa huwezi kubadilisha chochote,” alisema.

Alisema kikubwa kilichoibua shangwe kwa wabunge ni kitendo chake cha kuruhusu kushauriwa, kukosolewa na demokrasia nchini.

Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Rioba alisema hali ya uchumi kuwa ngumu katika kipindi hiki pia imechangia kuwafanya wabunge na watu wengine nje ya Bunge wamshangilie Kikwete.

“Pamoja na kujinasibu kuwa wamekusanya fedha nyingi, fedha za maendeleo zilizokwenda ni ndogo. Hali ni mbaya kila kona, wafanyabiashara na wafanyakazi hawapumui,” alisema.

Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salum alisema Kikwete alikuwa ni rahisi kufikika na alikuwa anasikiliza watu na mambo mengi alikuwa akiyatekeleza.

“Ukitaka kufahamu uzuri wa mtu, lazima ulinganishe watu wawili na ndicho kilichofanyika. Tulikuwa tunatumia njia ya kidemokrasia ya kutoka nje (ya ukumbi wa Bunge) wakati tukiwa na jambo ambalo halituridhishi,” alisema.

Mbunge wa Chambani (CUF) Yusuf Salim Hussein alisema Kikwete alikuwa anafanya vizuri lakini baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya vibaya.

“Chema chajiuza kibaya chajitembeza. Yule alikuwa akifanya kibaya kidogo, (hivyo) lazima ashangiliwe,” alisema.

Mbunge wa Konde (CUF), Said Haji Khatib alisema mapungufu ya Kikwete ni machache.

“Sisi wabunge wa upinzani tunamfagilia sana (Kikwete), anawajali watu wote, anashaurika na kukubali ushauri,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Pendo Peneza alisema Kikwete aliliacha Bunge kufanya kazi yake kwa uwazi bila kuliingilia, jambo ambalo liliifanya chombo hicho kuwajibisha viongozi pale ambapo inastahili kufanya hivyo.

Lakini wabunge wa CCM walisema shangwe hizo zinatokana na kutambua mchango wake.

“Kazi yake ni nzuri. Kwa mfano mimi sitamsahau kwa tabu tuliyokuwa tukipata katika kufika Tabora leo hii lami hadi Urambo. Kwanini tusifurahie?”alihoji mbunge wa Urambo (CCM), Magareth Sitta.

Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema watu wasifikirie tukio la kumshangilia Kikwete lina siasa ndani yake, bali ni la kawaida tu katika maisha inapotokea watu hawajaonana kwa muda mrefu.

“Kama hujamuona ndugu yako siku nyingi lakini ukaja kumuona lazima iwe hivyo kama leo,” alisema.

Kauli hiyo inalingana na ya mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillary aliyesema isingekuwa rahisi kwa wabunge kutomshangilia baada ya kuwaongoza kwa miaka kumi akiwa Ikulu.

“Ni kawaida ya kibinadamu kushangilia,” alisema Hillary.

Godluck Mlinga (CCM-Ulanga) alisema Kikwete bado anapendwa na wengi, wakiwemo wabunge.



Source: Mwananchi
Hii ndio sababu ya wabunge kumshangilia JK Hii ndio sababu ya wabunge kumshangilia JK Reviewed by Zero Degree on 4/05/2017 12:37:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.