Loading...

Jinsi tishio la mgomo wa Taboa lilivyosababisha mabasi yasafiri tupu

ZAIDI ya mabasi 30 jana yalikosa abiria na mengine kusafiri na watu wachache licha ya kusitishwa kwa mgomo wa mabasi yaendayo mkoani, nchi za jirani na usafiri wa daladala jijini Dar es Salaam.

Mgomo huo uliokuwa umeitishwa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (Taboa) kwa kushirikiana na Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar), uliahirishwa juzi baada ya vyama hivyo kufikia mwafaka na serikali.

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu akizungumza na Nipashe jana alisema abiria walikuwa wamejiandaa na mgomo huo wa nchi nzima na ndiyo sababu mabasi hayo yakakosa abiria na hivyo kubeba watu wachache au kushindwa kusafiri.

Alisema mabasi yaliyosafiri jana kwenda mikoa ya Mbeya, Arusha na Mwanza yaliondoka bila abiria na mengine yakashindwa kuondoka kabisa hali ambayo imewaathiri kiuchumi.

"Serikali isifikiri kuitisha mgomo ni kitu kidogo," alisema Mrutu ambaye ni mmliki wa kampuni ya Kirumo.

"(Mgomo) ni jambo kubwa na hali hii imesababisha leo (jana) tumekosa abiria wa kusafiri kwenda mikoa mbalimbali kwa sababu tulikuwa tumeshawatangazia kuwa hatutatoa."

Alisema zaidi ya mabasi 32 yalibaki Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) jana bila kusafiri. Aliainisha njia za mabasi hayo kuwa ni Arusha (zaidi ya 10), Mbeya (zaidi ya 10) na Mwanza (zaidi ya 12).

"Nashindwa kufahamu idadi kamili kwa sababu na mimi nimeondoka hapo asubuhi naelekea mkoani Arusha," alisema Mrutu, "ila mabasi ambayo hayajapata abiria ni mengi sana."

Aidha, katibu huyo alizitaka mamlaka kushughulikia makubaliano yao ili kuepuka usumbufu na adha ambazo serikali na wananchi wanaweza kuzipata kutokana na kuitishwa kwa migomo.

Alisema mgomo huo ulikuwa ukitaka kusababishwa na uzembe wa watendaji wasiotimiza wajibu wao wala kushirikiana na sekta hiyo ya usafiri katika kufanya maamuzi.

Alisema kama mgomo huo usingesitishwa ulikuwa ni mbaya kwa nchi kwa sababu walishaamua kutotoa huduma ya aina yoyote.

"Tanroads (Wakala wa Barabara), Polisi, Sumatra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) watimize wajibu wao kwa kufuata sheria zilizopo, (na) kwa kushirikiana na sisi kwa sababu tulitangaza kuwapo kwa mgomo siku ya Jumamosi na Jumapili serikali ilikuwa na uwezo wa kukaa na sisi, lakini walinyamaza kimya, hadi jana (juzi) tulipozungumza."

Kiongozi huyo aliwataka abiria kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida wakati Taboa na wadau wengine wakisubiri kufikia tamko la mwisho.

Taboa na Uwadar walitangaza mgomo wa kusafirisha abiria kuanzia jana, lakini ulisitishwa juzi baada ya vyama hivyo kukaa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

Mgomo huo ulikuwa ukihusisha mabasi yote ya abiria yaendayo mikoani na nchi za jirani na yale yanayosafirisha abiria jijini Dar es Salam, maarufu kama daladala, kupinga mabadiliko ya Sheria ambayo Sumatra imeyafanya.

Muswada wa sheria unaolalamikiwa na wamiliki hao unatarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya mwisho na kupitishwa kuwa sheria.

Kwenye muswada huo ambao wamiliki hao walisema hawakushirikishwa kwa hatua yoyote, iwapo dereva wa basi atafanya kosa, mmiliki wa basi atajumuishwa kwenye kesi husika mahakamani.

“Abiria watuwie radhi, lakini watambue kuwa athari watakazopata zinatokana na sheria kandamizi inayotaka kutungwa na Sumatra kuwakandamiza wenye mabasi na daladala," alisema Mrutu mwishoni mwa wiki iliyopita.

"Sheria hii ikipita hakuna mmiliki wa basi atakayeendelea na biashara hii hivyo kwa sauti moja tumeamua kugoma ili kupaza sauti zetu.”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa wamiliki hao walishirikishwa.

Alisema kulikuwa na kikao kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi mwezi uliopita na kwamba waliwapa siku 14 kuendelea kutoa maoni yao ili kuboresha kanuni za usafirishaji.
Jinsi tishio la mgomo wa Taboa lilivyosababisha mabasi yasafiri tupu Jinsi tishio la mgomo wa Taboa lilivyosababisha mabasi yasafiri tupu Reviewed by Zero Degree on 4/05/2017 11:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.