Loading...

Kisa cha binti wa miaka 16 kujitupa katikati ya Bahari

BINTI wa miaka 16 (jina linahifadhiwa kutokana na umri wake), aliyejitupa baharini kutoka kwenye 'boti' iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar jana asubuhi, alikuwa akirudishwa nyumbani kwa nguvu, imefahamika.

Msichana huyo aliokolewa na mabaharia wa boti aliyokuwa akisafira ya Kilimanjaro V inayomilikiwa na kampuni ya Azam Marine. 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini Zanzibar (ZMA), Abdallah Husein Kombo alisema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Azam Marine, binti huyo alipanda boti jana saa 3 asubuhi jijini Dar es Salaam akiongozana na wajomba zake wawili.

Mkurugenzi huyo aliwataja wajomba hao kuwa ni Hussein Abas na Omary Ally.

Kombo alisema kwa mujibu wa ripoti ya Azam, binti huyo mkazi wa Kikwajuni kwa Chile, aliondoka Zanzibar Ijumaa baada ya kugombezwa na wazazi wake.

Alisema kwa mujibu wa taarifa aliyopata kutoka Azam, binti huyo akiwa na Abas na Ally kwenye Kilimanjaro V na wakiwa katikati ya bahari aliomba kwenda kupunga hewa nje, akaruhusiwa na ndipo alipojitupa baharini baadaye.

Alipoulizwa juu ya chanzo cha ugomvi kati ya binti huyo na wazazi wake, Ally alikataa kuzungumza na kutaka waulizwe wazazi wa msichana.

Msichana huyo alijitupa baharini wakati boti hiyo ikiwa eneo la bahari ya Chumbe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema ilikuwa ni majira ya saa 5:15 asubuhi.

Alisema chanzo cha msichana huyo kujitupa baharini bado hakijajulikana kwa Jeshi la Polisi ambalo, hata hivyo, linaendelea na upelelezi.

Kamanda Ali alisema uchunguzi utakapokamilika, binti huyo atafunguliwa mahakamani shtaka la kutaka kujiua kwa makusudi.

“Ni kweli majira ya saa tano na robo asubuhi leo tumepokea taarifa ya mtu mmoja kujitupa baharini kwa makusudi akiwa safarini katika boti ya Kilimanjaro 'five',” alisema Kamanda huyo.

BAHARIA WA BOTI

Alisema manusura huyo alitaka kujiua kwa makusudi, lakini mabaharia wa boti hiyo walifanikiwa kumuokoa na kufikishwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu.

Muuguzi mfawidhi wa Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Fatma Mohammed Khamis alisema kuwa alimpokea manusura huyo majira ya saa 6:54 mchana akiwa katika hali mbaya.

Alisema baada ya kumpokea hospitalini hapo, walimpatia matibabu na hali yake ikarejea vizuri, lakini hakuwa na majeraha yoyote mwilini mwake.

“Kwa kweli alipofikishwa hospitalini hapa hali yake ilikuwa mbaya, lakini baada ya dakika 10 alipata nafuu na baadaye tumempa ruhusa ya kurejea nyumbani kwao” alisema muuguzi huyo.

Aidha, Fatma alisema licha ya kutopata majeraha yoyote, lakini anaonekana kuwa na tatizo la saikolojia hivyo alishauri ni vyema akapatiwa ushauri nasaha.

Ni mara ya kwanza kwa abiria wa boti au meli zinazofanya safari zake kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, mwendo wa saa mbili baharini, kujirusha kwenye maji kwa nia ya kijiua.

Source: Nipashe
Kisa cha binti wa miaka 16 kujitupa katikati ya Bahari Kisa cha binti wa miaka 16 kujitupa katikati ya Bahari Reviewed by Zero Degree on 4/04/2017 11:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.