Loading...

Simba mambo si shwari

UKISEMA mambo si shwari Simba utakuwa hujakosea, kutokana na kuanza kutafutana uchawi baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar juzi, wakifungwa mabao 2-1, ukichezwa Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera.

Wekundu hao wa Msimbazi ambao waliongoza Ligi kwa muda mrefu, walijikuta wakishushwa na watani zao wa jadi, Yanga na sasa watatakiwa kupambana kisawasawa ili kushinda michezo yao yote iliyobakia, huku wakiwaombea mabaya Wanajangwani hao, la sivyo ubingwa watausikia tu mitaani.

Katika mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar, mabao ya wenyewe wao hao yalipachikwa wavuni na Mbaraka Yusuph pamoja na Edward Christopher, wachezaji ambao walilelewa na Simba tangu wakiwa kikosi B.

Kutokana na ushindi huo wa Kagera, Yanga wamerudi kileleni wakiwa na pointi 56, huku Simba wakibakia nafasi ya pili na pointi zao 55, kitu ambacho kinawafanya baadhi ya mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, kupandwa na jazba.

Baada ya kujikuta wakiangukia kipigo hicho, tayari bundi ameanza kulia kwa Wekundu hao wa Msimbazi, wakitafuta mchawi ambapo taarifa zinadai kuwa, wapo baadhi ya wachezaji wanashutumiwa kucheza chini ya kiwango na kusababisha kufungwa.

Taarifa hizo zinadai kuwa, huenda wachezaji hao ambao wanahisiwa kucheza chini ya kiwango wakapigwa chini wasionekane tena hata michezo inayokuja, huku pia ikisemekana kuna baadhi ya viongozi nao wanachunguzwa mwenendo wao.

Kutokana na mtikisiko huo, taarifa zisizo na shaka ambazo zinasema kuwa, hata kwenye yale makundi ya kijamii kama WhatsApp, baadhi ya watu wameanza kuondolewa kwa kisingizio cha kuihujumu timu na kuonekana hawana msaada wowote.

Kwa sasa Simba wanakabiliwa na michezo mingine miwili ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Mbao FC pamoja na Toto Africans, ambapo baadhi ya wadau wa soka wanadai kuwa, kama wataanza kutafuta mchawi watapotea kabisa kwenye mbio za ubingwa, ikizingatiwa kuwa kufungwa ni jambo la kawaida.

Mbali na michezo hiyo ya Kanda ya Ziwa, michezo mingine ambayo Wekundu hao wa Msimbazi wamebakisha ni dhidi ya African Lyon, Stand United pamoja na Mwadui, yote ikitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Source: Bingwa
Simba mambo si shwari Simba mambo si shwari Reviewed by Zero Degree on 4/04/2017 12:32:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.