Loading...

Uganda kuunda magari yake

Picha ya Mtandao
KATIKA kuhakikisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinapunguza uagizaji wa magari kutoka nje, Uganda iko mbioni kuungana na nchi nyingine za EAC za Tanzania, Kenya na Rwanda katika ujenzi wa viwanda vya kisasa, vikiwemo vinavyotengeneza na kuuza nje ya nchi magari ya kubeba watalii, malori ya takataka na pikipiki za aina mbalimbali.

Kwa Uganda inayoagiza wastani wa magari 50,000 kwa mwaka, huo ulikuwa mpango wa muda mrefu na sasa umeiva baada ya Rais Yoweri Museveni kuingilia kati na kuagiza kazi za ujenzi wa kiwanda ianze mara moja.

Tayari Baraza la Mawaziri kupitia kikao chao, kilichoongozwa na Rais Museveni kimeiagiza Wizara ya Fedha kutenga dola za Marekani milioni 5.6 ambazo ni sawa na shilingi za Uganda bilioni 20 katika mwaka ujao wa fedha ili shughuli za ujenzi wa kiwanda hicho uanze.

Wazo la ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji wa magari, lilianza nchini Uganda mwaka 2011 baada ya juhudi na maarifa ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere kutengeneza gari, linalotumia umeme la Kiira EV na linalotumia nishati ya jua la Kayoola EV mwaka 2016.

Kutokana na mafanikio hayo ya wanafunzi wa Chuo kikubwa barani Afrika, mwaka 2014 serikali ilitenga kipande cha ardhi Mashariki mwa Jinja kwa ajili ya kiwanda cha magari kiitwacho Kiira Motors Corporation na kampuni iliyopewa kandarasi ya kujenga kiwanda hicho ni kutoka China ya China Engineering Limited.

Malengo makuu yaliyowekwa wakati huo ni kuwa ikifika mwaka huu uzalishaji wa magari, uwe umeanza na gari la kwanza lizinduliwe na Rais Museveni.

Mradi huo mkubwa katika historia ya Uganda, unatarajiwa kutengeneza nafasi za ajira za moja kwa moja zaidi ya 2,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 12,000.

Kiwanda hicho kitakapokamilika na kuanza uzalishaji wa magari, Uganda itapata soko kubwa katika nchi za Afrika Mashariki kutokana na mahitaji makubwa ya magari.

Afrika Mashariki huagiza magari 250,000 kwa mwaka na mahitaji yanatarajiwa kupanda hadi kufikia magari 500,000 kufikia mwaka 2030.

Magari ya Tanzania Kampuni ya Hanspaul Automechs Limited (HAL) iliyopo eneo la viwanda Njiro jijini Arusha, inatengeneza magari makubwa ya kubeba watalii maarufu kwa jina la ‘War Bus’.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul, yanauzwa Kenya, Afrika Kusini na nchi za Ulaya.

Kampuni hiyo imebuni na kutengeneza pia magari maalumu ya kubeba taka, yanayofaa kwa mazingira ya Tanzania, ikiwemo hali ya hewa, aina ya barabara na mfumo wa maisha wa wananchi wake.

“Lakini aina mpya ya malori ya kubeba takataka si kwa ajili ya kampuni yetu au kiwanda chetu tu, kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania), wazalishaji wengine wanaweza kuyatengeneza lakini kwa kutumia utambulisho wa ubunifu wa HAL kama kielelezo,” alisema Hanspaul.

Alisema, magari ya kubeba takataka na yale ya watalii ni ubunifu wa Tanzania unaozivutia nchi nyingine zikiwemo za Ulaya na magari ya watalii yanakubalika kwenye soko la kimataifa. Kwa mwezi huweza kutengeneza zaidi ya magari 35.

Watu wengi hawataamini kwamba, nchi zenye viwanda vya kutengeneza magari kama Afrika Kusini na zile za Ulaya sasa zinanunua magari kutoka Tanzania, lakini wanafanya hivyo,” alisema.

Magari hayo yenye nembo za Toyota, Nissan na Land Rover, yanatengenezwa kwa kutumia mashine za kisasa zikiwemo roboti kama ilivyo kwenye viwanda vya magari katika nchi zilizoendelea. HAL ilianzishwa mwaka 2007 na imelenga kuteka asilimia 25 ya soko la magari na spea zake katika nchi za EAC.

“Tuna kila kitu kinachohitajika, mitaji kutoka kwenye taasisi za benki, intaneti yenye kasi, mawasiliano ya simu, nguvukazi ya kutosha na ardhi ya kutosha, tunachohitaji sasa ni watu kubadili mitazamo yao,” alisema Hanspaul.

Kenya, Uganda na Afrika Kusini wanatumia ‘War Bus’ kupeleka watalii kwenye hifadhi za taifa na kuna taarifa zinazodai kuwa baadhi ya nchi zinayatumia kwenye shughuli za kijeshi.

Volvo yaingia Kenya

Moja ya kampuni kubwa katika utengenezaji wa magari ya aina mbalimbali, Volvo imeingia nchini Kenya na kuwekeza Shilingi bilioni 2.5 za nchi hiyo ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda kinachotarajiwa kuanza na uzalishaji wa magari 500 kwa mwaka na baadaye kufikia magari 2,000 kwa mwaka.

Kiwanda hicho kilichoingia ubia na kampuni ya NECST Motors ya Kenya, kinatarajiwa kuzalisha ajira 300 za moja kwa moja kiwandani hapo, lengo likiwa kushika asilimia 20 ya soko la Afrika Mashariki. Ni kiwanda cha tatu barani Afrika, vingine vikiwa Morocco ambako imeshika asilimia 20 ya soko na Afrika Kusini inakoshika asilimia 18 ya soko la magari.

Kwa Kenya, kitakuwa kiwanda cha nne cha magari.

Volkswagen kimeanza tena kazi baada ya kusitisha uzalishaji miaka 40 iliyopita. Kampuni za Peugeot, Toyota, wameanza pia uzalishaji, huku Iveco, Ashok Leyland pia wakitangaza nia ya kuanza uzalishaji wake nchini Kenya.

Gari la kwanza Rwanda Gari la kwanza litakalotengenezwa Rwanda linatarajiwa kuingia barabarani mwezi ujao. Hiyo ni mali ya kampuni ya Volkswagen (VW) ya Ujerumani ambayo iko katika maandalizi ya kutengeneza aina tatu za magari madogo nchini humo, ya Volkswagen Passat, Volkswagen Polo na Volkswagen Teramont.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa VW nchini Afrika Kusini, Thomas Schafer mwanzoni mwa mwaka huu alisema uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 20 ni matunda ya upembuzi yakinifu uliofanywa na kuonekana ni mradi `utakaolipa’ kwa nchi za EAC.

Aliongeza kuwa, licha ya kwanza wanafanya pia uwekezaji nchini Kenya, aina ya bidhaa zitatofautiana ili kupanua wigo wa soko. Nchini Rwanda wanakotarajia kuzalisha magari 5,000 kwa mwaka, ajira zinazotarajiwa kuzalishwa n kati ya 500 na 1,000.

Pikipiki Nchi ya Rwanda, Kampuni ya Pikipiki Rwanda (RMC) kuanzia mwaka jana imeanza kutengeneza aina mbalimbali za vyombo hivyo vya usafiri na tayari soko lake limeanza kukua katika nchi jirani, zikiwemo Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mauzo RMC, Luois Masengesho wanatengeneza aina saba za pikipiki zikiwemo Ingenzi, Indakangwa, Indahigwa, Imparage, Infarasi na Inzovu.

Kila pikipiki inauzwa kwa kati ya Faranga za Rwanda milioni 1.2 hadi Faranga milioni 3 kwa kuzingatia uwezo wa injini na ukubwa zikiwemo za CG250 na CG125. Kwa mujibu wa Masengesho, walengwa wakubwa wa pikipiki hizo ni wafanyabiashara wa bodaboda, wanaozitumia kwa ajili ya michezo, maofisa wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.

“Tunashukuru soko limetupokea vizuri na kwa sababu ya nia iliyooneshwa kwenye nchi hizi (Tanzania na DRC) tunatarajia kuongeza mauzo,” alisema Masengesho.
Uganda kuunda magari yake Uganda kuunda magari yake Reviewed by Zero Degree on 4/17/2018 11:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.