Loading...

Kijana apewa kazi na uraia nchini Ufaransa kwa kumuokoa mtoto ghorofani


Kijana mmoja ambaye ni mhamiaji nchini Ufaransa kutoka nchini Mali amepata shavu la kuonana na Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron katika Ikulu yake ya Elysee leo (Mei 28, 2018).

Kijana huyo aitwae Mamoudou Gassam amepata heshima hiyo baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akimwokoa mtoto aliyekuwa akining’inia ghorofani.

Video hiyo ambayo ilichukuliwa na moja ya mashuhuda wa tukio hilo ilimuonesha kijana huyo akipanda jengo hilo lililopo jijini Paris hadi kufikia ghorofa ya nne kupitia vibaraza, mpaka kumfikia mtoto huyo aliyekuwa amenasa kwenye chuma cha uzio.


Baada ya tukio hilo, kijana huyo wenye umri wa 22 akawa gumzo si tu Jijini Paris, bali duniani kwa ujumla baada ya video kusambaa, shukrani kwa maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Taarifa hii ikamfikia Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Ndipo Ikulu ikatoa taarifa rasmi ya kumpongeza kisha kumwalika Ikulu kijana huyo kwa ushujaa aliouonesha.

Kwa upande wa Meya wa jiji la Paris, lilipotokea tukio hilo, Anne Hidalgo, pia amempongeza kijana huyo akisema “Hongera kwa Mamoudou Gassama kwa kitendo chake cha kishujaa kilichookoa maisha ya mtoto”

Ameongeza kuwa amekwisha mpigia simu Gassama kumshukuru na kuahidi kwamba atamsaidia kupata uraia wa nchi hiyo ili aanze maisha jijini Paris, ambako amefika miezi michache iliyopita kutoka Mali. Hata hivyo, ahadi hiyo hiyo ilitekelezwa mara moja kwani imethibitika kuwa ameshapewa uraia na zaidi ya yote, kijana huyo amepewa ajira katika kikosi cha Zimamoto, jijini Paris.

Gassama akizungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa alipoona mtoto ananing’inia ghorofani na watu wakipiga kelele na kushangaa, alifikiria suluhisho la tatizo.

Anasema “ndio maana niliamua kupanda zile ghorofa, namshukuru Mungu, yeye ndiye aliyemuokoa”
Kijana apewa kazi na uraia nchini Ufaransa kwa kumuokoa mtoto ghorofani Kijana apewa kazi na uraia nchini Ufaransa kwa kumuokoa mtoto ghorofani Reviewed by Zero Degree on 5/29/2018 08:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.