Loading...

Rais ateua ndugu wanne wa familia yake kuwa majenerali jeshini


RAIS Teodoro Obiang Nguema, wa Equatorial Guinea amewateua ndugu wanne wa familia yake kuwa majenerali katika Jeshi la nchi hiyo.

Nguema anayetawala taifa hilo dogo magharibi mwa Afrika lenye utajiri wa mafuta na chuma, amefanya uteuzi huo Oktoba 12 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.


Pia ameteua mwanaye, Teodorin Nguema Obiang, kuwa meja-jenerali. Mwanaye huyo ambaye ni mtoto wake pekee wa kiume pia ndiye makamu wa kwanza rais wa taifa hilo. Aliteuliwa kuwa makamu wa pili wa rais mwaka 2012 kabla ya mwaka 2016 kuwa makamu wa kwanza na ndiye anayetajwa kumrithi baba yake katika kiti cha urais.

Sambamba na huyo, Nguema pia amemteua shemeji yake aitwaye Victoriano Nsue Okomo kuwa meja jenerali kutoka kanali, akiruka cheo cha brigedia jenerali. Pia amemteua mtoto wa dada yake, Jose Eneme Obama, kuwa brigedia jenerali kutoka mrja akiruka vyeo viwili juu yake (luteni kanali, na kanali).

Pia amempandisha cheo mkwe wake (mume wa mwanaye) aitwaye Fausto Abeso Fuma kutoka luteni kanali hadi brigedia jenerali na kumteua kuwa mkuu wa kamandi ya anga katika jeshi la nchi hiyo.

Nguema alichukua madaraka ya nchi hiyo mwaka 1979 baada ya kumpindua mjomba wake Francisco Macías Nguema akimtuhumu kuongoza nchi hiyo kimabavu na kutumia vibaya fedha za umma. Ameongoza taifa hilo kwa miaka 39 na kuweka rekodi ya rais aliyepo madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Anashutumiwa kuongoza nchi hiyo kidikteta, kuminya uhuru wa maoni na kukandamiza demokrasia. Anatuhumiwa pia kwa matumizi mabaya ya fedha za umma kutokana na familia yake kumiliki majengo ya kifahari mjini Paris, Ufaransa.

Septemba 17 mwaka huu, mwanaye ambaye ni Makamu wa kwanza wa Rais, Teodorin Nguema Obiang, alikamatwa na dola milioni 16 pesa taslimu (sawa na Sh. bilioni 35 za Tanzania) huko Brazil zikiwa kwenye mabegi.

Nchi hiyo ina idadi ya watu milioni moja na laki mbili, ambapo asilimia kubwa ya watu wake wanaishi kwenye umaskini wa kupindukia wa chini ya dola moja kwa siku. Ina chuo kikuu kimoja tu cha umma na huduma za afya, maji na elimu ni duni sana.

Mwaka 2008 shirika la Afya Duniani (WHO) lilieleza kuwa nchi hiyo ilikadiriwa kuwa na madaktari 140, manesi 400, wafamasia 20 na madaktari bingwa 10 tu!
Rais ateua ndugu wanne wa familia yake kuwa majenerali jeshini Rais ateua ndugu wanne wa familia yake kuwa majenerali jeshini Reviewed by Zero Degree on 10/24/2018 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.