Loading...

Mjadala waibuka uteuzi wa Raila Odinga AU


SIKU moja tu baada ya Umoja wa Afrika (AU) kutangaza kumteua kinara wa upinzani ndani ya muungano wa NASA ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga, katika wadhifa wa msimamizi wa ujenzi wa miundo msingi barani Afrika, mjadala umeibuka kama ni wakati mwafaka kustaafu siasa.

Wanaoshadadia Raila kustaafu ni baadhi ya viongozi wa Chama cha Jubilee ambao katika mikutano tofauti ya siasa mwishoni mwa wiki iliyopita, walimtaka kiongozi huyo wa ODM kujikita zaidi kwenye majukumu yake mapya na kuachana na siasa za Kenya.

Ni dhahiri Raila bado ni tishio kuelekea uchaguzi mkuu 2022 ingawa bado hajaweka wazi kama atagombea. Baadhi ya viongozi wa Jubilee hususan kutoka sehemu anayotoka Naibu Rais William Ruto wanamuona Raila kama kikwazo kwa azma ya Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Aidha wanaona shinikizo la Raila kubadilisha baadhi ya vipengele katika Katiba yanalenga kumwondoa Ruto ambaye ameweka wazi nia yake ya kuwa Rais wa tano wa Kenya.

Kitendo cha Raila na Uhuru kukubali kufanya kazi pamoja, nacho wamekitafsiri kumwekea Ruto mazingira magumu kutimiza ndoto yake ya urais.

Hivyo basi uteuzi wa Raila AU umepokelewa kwa hisia tofauti hususan na wanasiasa huku macho yote yakielekezwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Raila aliteuliwa na Mwenyekiti wa AU, Moussa Faki, ambaye katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema kiongozi huyo wa ODM atashirikiana na umoja huo kuimarisha juhudi zake katika miundo msingi.

Akihutubia taifa katika Sikukuu ya Mashujaa iliyoadhimishwa Jumamosi iliyopita Uwanja wa Bukhungu kaunti ya Kakamega, Rais Uhuru alimpongeza Raila kwa uteuzi huo na kusisitiza asingeweza kufanikiwa iwapo wasingekubali kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wananchi.

Aidha ameongeza uteuzi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwa sababu wakati Raila atakapokuwa akiongoza kitengo hicho, hatasahau changamoto zinazokumba Kenya katika masuala ya miundo msingi.

“Tunapokuja pamoja, tunapata fursa kufaidika zaidi. Sasa mnaona ndugu yetu amepata kazi AU na anayefaidika zaidi ni sisi Wakenya,”alisema Rais Uhuru.

Alisema uteuzi wake huo mpya utasaidia serikali yake kutimiza malengo nne kuu (Big Four Agenda) yanaolenga miundombinu na ustawi wa maendeleo ya nchi.

“Raila atafanya kazi kwa karibu na serikali yangu kuhakikisha anatenga rasilimali nyingi kwa Kenya ili tufanikishe maono ya 2030 (Vision 2030). Tumetengeza historia kama nchi na Kenya ina nafasi kufaidika zaidi baada ya makubaliano yetu kufanya kazi pamoja,”alisema Uhuru.

Rais Uhuru amekuwa katika mstari wa mbele kufanikisha Raila anateuliwa AU na inadaiwa mpango huo ulikubaliwa miezi sita iliyopita.

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Monica Juma, alisema makubaliano ya uteuzi huo yalifikiwa Aprili mwaka huu baada ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Faki, alipomtembelea Rais Uhuru Ikulu jijini Nairobi.

Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Erastus Mwencha, aliyestaafu mwaka jana alidokeza nafasi hizo nyeti kama aliyopewa Raila mara nyingi zinakubaliwa na marais mbalimbali kabla ya rais wa nchi husika kubariki pendekezo hilo.

“Mara nyingi uongozi wa AU wanakubaliana kwa mtu wanayemuona ni sahihi kabla ya kupata ushauri kutoka kwa rais wa nchi husika anakotoka mgombea mteule. Hivi ndivyo huenda ilivyotokea katika kesi ya uteuzi wa Raila,”alisema Mwencha.

Kama balozi mteule wa Mwenyekiti wa AU, Raila atakuwa na ofisi jijini Addis Ababa, Ethiopia lakini atakuwa anasafiri maeneo mbalimbali ndani ya bara la Afrika. Atashiriki katika mijadala ya amani na usuluhisho wa migogoro. Raila pia atakuwa na ofisi iliyokamilika jijini Nairobi, wafanyakazi na washauri kuhakikisha uwepo wake nchini na ushirikiano na Rais Uhuru.

Ni vigumu kutenganisha uteuzi wa Raila na siasa za Kenya na hakuna dalili za yeye kukaa pembeni, hivyo tutarajie akitumia muda wake vizuri kuhudumu majukumu yake mapya na kuendelea na siasa za Kenya.

Itakuwa vigumu Raila kuachana na siasa kwani imekuwa jambo la kawaida kwa wanasiasa kuendelea kupiga siasa licha ya wadhifa walinazo. Baadhi ya viongozi wa Jubilee wanaotaka Raila kuacha siasa ili atumikie kazi yake mpya wanasahau na wao badala ya kuendeleza ajenda nne za Rais Uhuru, wamekuwa wakipiga siasa za kuelekea 2022.
Mjadala waibuka uteuzi wa Raila Odinga AU Mjadala waibuka uteuzi wa Raila Odinga AU Reviewed by Zero Degree on 10/24/2018 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.