Loading...

Polisi yaja na takwimu zao mauaji mkoani Kigoma


SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kuibua tuhuma za mauaji ya wananchi zaidi 100 katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno, amesema taarifa hizo hazina ukweli.

Kamanda Ottieno alisema ukweli uliopo ni kwamba askari wawili na wananchi wawili ndiyo waliopoteza maisha katika mapigano ya jamii ya wafugaji.

Juzi, Zitto aliwaambia waandishi wa habari kuwa mauaji hayo yalitokea kwenye mapigano kati ya polisi na Wanyantuzu wilayani Uvinza, takribani siku 11 zilizopita.

Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, alidai kuwa katika tukio hilo mbali na wananchi 100 kupoteza maisha pia askari wawili waliuawa.

Kwa mujibu wa gazeti la MTANZANIA, Kamanda Ottieno alisema Zitto amezungumza upotoshaji na anatafuta umaarufu kupitia tukio hilo hivyo apuuzwe.

“Zitto anazungumza upotoshaji, ni mwongo anatafuta kiki ambazo hazina maana, wananchi wapuuze taarifa yake,”alisema Kamanda Ottieno.

Alipoulizwa endapo hakuna hata mwananchi mmoja aliyefariki katika mapigano hayo, alisema ni wananchi wawili na askari wawili tu waliopoteza maisha.

“Ni kweli askari wawili waliuliwa na jamii hiyo ya wafugaji katika mapigano hayo na ni wananchi wawili tu ndiyo waliofariki na sio 100 kama anavyopotosha Zitto,”alisema kamanda huyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema taarifa za wananchi 100 kuuawa si za kweli na kwamba kwa sasa anasubiri taarifa kutoka kwa Inspekta Generali wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

“Sina taarifa za aina hiyo, lakini kuna askari wetu wawili walipoteza maisha na IGP yuko kule tunasubiri atuletee taarifa,”alisema Lugola.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi, Zitto alisema wiki iliyopita yalitokea mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mto Malangarasi, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi wenye hasira.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno.

“Kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yoyote kwa wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mpeta,”alisema Zitto.

Kutokana na hilo, alisema chama chao kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi taarifa hizo.
Polisi yaja na takwimu zao mauaji mkoani Kigoma Polisi yaja na takwimu zao mauaji mkoani Kigoma Reviewed by Zero Degree on 10/30/2018 09:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.